Ronaldo ampigia Jose Mourinho upato kuwa kocha wa timu ya taifa ya Brazil

Kulingana na nyota huyo, wakati umefika Brazil kujaribu huduma za kocha raia wa kigeni.

Muhtasari

• Nyota huyo aliwataja makocha wengine ambao anawapigia upato kung'ang'ania nafasi ya ukufunzi Brazil.

• Kocha Tite aling'atuka kama kocha baada ya Brazil kubanduliwa nje ya kombe la dunia katika mechi ya kufuzu nusu fainali dhidi ya Croatia.

Mourinho apigiwa upate kuwa kocha wa Brazil
Mourinho apigiwa upate kuwa kocha wa Brazil
Image: Hisani

Mkongwe wa soka kutoka Brazil Ronaldo Nazario ametoa tamko lake kuhusu ni nani anayefaa kuchukua nafasi ya kocha Tite ambaye aling’oka madarakani kama kocha wa timu ya taifa ya Brazil baada ya kushindwa kuisaidia timu hiyo kufuzu nusu fainali dhidi ya Croatia.

Kulingana na Metro UK, Nazario alisema ni wakati sasa viongozi wa soka Brazil kutathmini kumpa raia ambaye si wa taifa hilo kazi ya ukufunzi ili waweke hai matumaini yao ya kushinda mataji makubwa katika malimwengu ya soka na kurudisha fahari yao ya zamani enzi akina Ronaldo Nazario wakiwa wachezaji hatari.

Ronaldo alitoa orodha yake ambayo anadhani ni watu wanaofaa kuzingatiwa katika orodha ya watakaohojiwa kuchukua nafasi ya Tite huku akiwataja makocha nguli kama kocha wa Roma Jose Mourinho miongoni mwa majina mengine makubwa.

“Kuna majina mengi ya kushangaza ambayo yangefanya mema mengi.  Ancelotti, Abel Ferreira, kutoka Palmeiras, Jose Mourinho, kutoka Roma ni miongoni mwa wale ninaowapigia upato. Sijui nin ishirikisho la soka Brazil litafanya lakini nahisi ni muda wa kutafuta kocha wa kigeni,” Metro UK walimnukuu.

Brazil walitimuliwa katika robo-fainali baada ya kushindwa na Croatia waliofuzu fainali za Kombe la Dunia 2018. Sare ilibidi iamuliwe kupitia kwa mikwaju ya penalti, huku vijana wa Tite wakipoteza 4-2 baada ya Marquinhos na Rodrygo kushindwa kufunga mikwaju yao ya Penalti.