Kombe la Dunia 2022: Fifa inachunguza Salt Bae ‘alivyofika uwanjani’ baada ya fainali

"Hatua ifaayo ya ndani itachukuliwa." FIFA imesema.

Muhtasari

•Salt Bae alionekana katika picha akiwa ameshika na kubusu kombe la Kombe la Dunia akisherehekea na wachezaji wa Argentina baada ya ushindi wao dhidi ya Ufaransa.

Salt Bae akiwa ameshika Kombe la Dunia
Image: HISANI

Fifa inachunguza jinsi mpishi maarufu Salt Bae na watu wengine kadhaa walipata "nafasi isiofaa" kufika uwanjani mwishoni mwa fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar.

Salt Bae, mpishi wa Uturuki ambaye jina lake halisi ni Nusret Gokce, alionekana katika picha akiwa ameshika na kubusu kombe la Kombe la Dunia akisherehekea na wachezaji wa Argentina baada ya ushindi wao dhidi ya Ufaransa.

Sheria za Fifa zinasema kombe hilo linaweza tu kushikiliwa na kundi la watu "walioidhinishwa", wakiwemo washindi wa mashindano, maafisa wa Fifa na wakuu wa nchi.

Katika taarifa kwa BBC Sport, msemaji wa Fifa alisema: "Baada ya tathmini, Fifa imekuwa ikibaini jinsi watu binafsi walivyoweza kuingia uwanjani baada ya sherehe za kufunga michuano hiyo katika uwanja wa Lusail mnamo Desemba 18.

"Hatua ifaayo ya ndani itachukuliwa."

Salt Bae anamiliki msururu wa maduka ya kifahari ya nyama na alijipatia umaarufu mwaka wa 2017 baada ya mbinu yake ya kuandaa na kutia chumvi kwenye nyama kuwa meme mtandaoni.

Wanasoka wengi wa sasa na wa zamani, akiwemo Messi, Cristiano Ronaldo na David Beckham, wamekula kwenye migahawa ya Salt Bae.

Mnamo Novemba, wakati wa Kombe la Dunia, alichapisha video akimkumbatia rais wa Fifa, Gianni Infantino, ambaye baadaye alipigwa picha kwenye viti vya watu mashuhuri kwenye mchezo na nguli wa Brazil Ronaldo, Roberto Carlos na Cafu.