Brighton wamfanya Mwepu, 24, kuwa kocha baada ya kustaafu kutokana na matatizo ya Moyo

Raia huyo wa Zambia alilazimika kustaafu kucheza soka baada ya kupatikana na ugonjwa wa moyo.

Muhtasari

• Mwepu sasa atakuwa anawanoa vijana wasiozidi umri wa miaka 9 katika akademia ya Brighton & Hoven.

Enock Mwepu, kiungo wa Brighton
Enock Mwepu, kiungo wa Brighton
Image: Facebook

Aliyekuwa kiungo wa Brighton Enock Mwepu na ambaye alilazimika kustaafu kucheza soka akiwa na umri wa miaka 24 tu kufuatia ugonjwa wa moyo hatimaye nyota yake imeng’aa tena.

Mwepu, raia wa Zambia mwenye umri wa miaka 24 alitangaza kustaafu miezi michache iliyopita baada ya kupatikana na matatizo ya moyo ambayo daktari walisema hangeweza tena kuendelea kukimbia uwanjani.

Klabu ya Brighton & Hoven ambayo alikuwa akichezea mpaka kupata taarifa hizo za kushtusha sasa imeripotiwa kumpa nafasi ya pili Mwepu kwa kumteua kuwa kocha wa vijana wasiozidi umri wa miaka 9 katika klabu hiyo ya Uingereza.

Alicheza muda mwingi wa uchezaji wake katika klabu ya RB Salzburg kabla ya kujiunga na timu ya Premier League kwenye dirisha la usajili la majira ya kiangazi mwaka 2021 kwa ada ya Euro milioni 23.

“Kwa kuwa hawezi kucheza soka tena, ameamua kwenda kufundisha na ameanza safari yake mpya kama kocha wa akademi ya Brighton's under 9's akiambatana na klabu iliyomleta kwenye Premier League,” Jarida la Vanguard liliripoti.

Aliitwa "kompyuta" kama jina la utani wakati wa utoto wake na wakati wa kucheza kwa sababu ya akili yake wakati akicheza mpira. Alikuwa Nahodha wa timu ya taifa ya Zambia ya "Chipolopolo boys" kabla ya kustaafu.

Baada ya habari hizo kuthibitishwa na klabu, Mwepu alitweet:

“Mpango wa Mungu na wakati wake daima ni kamilifu. Kumaliza mwaka kwa furaha. mimi ni wa Kristo Yesu.”