Cristiano Ronaldo:Nimeimaliza kazi yangu Ulaya

Mshambuliaji alikuwa na "ofa nyingi" kutoka kwa vilabu vingine.

Muhtasari

•Alijiunga na Al Nassr baada ya kuondoka Manchester United kufuatia mahojiano yenye utata ambapo aliikosoa klabu hiyo.

Image: BBC

Cristiano Ronaldo anasema kazi yake barani Ulaya imekamilika, lakini alikuwa na "nafasi nyingi" kutoka kwa vilabu vingine kabla ya kujiunga na Al Nassr ya Saudi Arabia.

Alijiunga na Al Nassr kama mchezaji huru siku ya Ijumaa baada ya kuondoka Manchester United kufuatia mahojiano yenye utata ambapo aliikosoa klabu hiyo.

Nahodha huyo wa Ureno, 37, alisema alikuwa na ofa kutoka kwa vilabu vya Brazil, Australia, Marekani na Ureno.

"Nilitoa ahadi yangu kwa klabu hii," alisema wakati wa uzinduzi wake Jumanne.

"Nilishinda kila kitu, nilichezea vilabu muhimu zaidi barani Ulaya na sasa ni changamoto mpya barani Asia."

Ronaldo anaripotiwa kupokea mshahara mkubwa zaidi katika historia ya soka wa zaidi ya £177m kwa mwaka katika mkataba unaoendelea hadi 2025.

"Kama hakuna anayejua, naweza kusema sasa nilikuwa na fursa nyingi Ulaya, vilabu vingi nchini Brazil, Australia, Marekani, hata Ureno, vilabu vingi vilijaribu kunisajili," Ronaldo aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wake wa kwanza na wanahabari.