Arsenal wakiendelea hivi hatutawafikia, huenda wakapita pointi 100 - Pep Guardiola

Guardiola alisema ubora Arsena unawapa nafasi ya kufikisha pointi zaidi ya 100.

Muhtasari

• Licha ya kukiri kuwa Arsenal ni timu nzuri, Guardiola alisema watajitahidi ili kuwang'atua kileleni mwa jedwali, huku akitumai watapoteza pointi.

Guardiola aipigia upato Arsenal kufika pointi 100
Guardiola aipigia upato Arsenal kufika pointi 100
Image: Maktaba

Mkufunzi wa Manchester City Pep Guardiola amefunguka wasiwasi wake kuhusu ligi ya Premia ya Uingereza huku timu yake wakijiandaa Alhamisi hii usiku kumenyana na Chelsea wakijaribu kubana mwanya kati yao na viongozi Arsenal.

Katika mahojiano na wanahabari mbele ya mechi hiyo ya Stamford Bridge, Guardiola aliuliziwa kuhusu Arsenal na uwezekano wao kushinda ubingwa wa ligi ya Premia msimu huu.

Guardiola alikiri kuwa vijana wa Arteta wako imara msimu huu kinyume na misimu ya nyuma na kusema wakiendelea na uzuri wao ambao wako nao kwa sasa, basi itakuwa vigumu kwa timu yoyote, ikiwemo Man City kuing’atua Arsenal kileleni mwa jedwali.

Alisema kuwa wakiendelea hivyo huenda watafikisha pointi zaidi ya 100 kwenda mbele na kuandikisha rekodi mpya, akisema kuwa ushindi wao katika mechi zilizopita unaonesha kuwa wako katka uwastani wa kufikisha pointi hizo.

“Arsenal wana wastani wa kufikisha pointi 100 - au zaidi ya pointi 100. Wakiendelea hivyo, hatutawapata,” Guardiola mwenye wasiwasi wa kutetea ubingwa huo kwa mara ya tatu mtawalia alisema.

Licha ya kuwapa Arsenal asilimia kubwa ya kushinda ligi hiyo, Guardiola alisisitiza kuwa vita bado vingalipo na mapambani yataendelea mpaka tone la mwisho la jasho huku akisema kuwa timu yake wanajitahidi kuwa karibu na uzuri kama wa Arsenal ili kuwapa kibarua kigumu kileleni.

“Kwa hivyo inabidi tuwe wakamilifu kuanzia hapa hadi mwisho wa msimu na kutumaini kwamba watashuka kidogo katika viwango vyao,” alisema.