Mmiliki wa Chelsea Todd Boehly ajiuzulu kama msimamizi wa usajili wa wachezaji

Baada ya kuinunua Chelsea mwaka jana, Boehly alijipa mamlaka ya kusimamia kusaini wachezaji wapya.

Muhtasari

• Wadhifa wa uhamisho na usajili wa wachezaji ulikuwa umeshikiliwa na Marina Granovskaia pamoja na Peter Cech ambao wote waling'atuka.

Mmiliki wa Chelsea Todd Boehly amejiuzuu
Mmiliki wa Chelsea Todd Boehly amejiuzuu
Image: Chelsea News

Mmiliki wa timu ya Chelsea Todd Boehly ameripotiwa kujiuzulu wadhifa aliokuwa ameshikilia kikaimu kama msimamizi wa kutambua na kusajili wachezaji wapya katika timu hiyo.

Mwaka jana baada ya kuinunua timu hiyo kutoka kwa bilionea wa Urusi Roman Abrahamovic, Boehly alijitwika jukumu la kuwa mkurugenzi wa kuangalia na kusajili vipaji vipya katika Chelsea na inadiwa kuwa yeye ndiye aliongoza kusajiliwa kwa wachezaji kama Pierre Emerick Aubameyang, Marc Cucurela, Kalidou Koulibaly pamoja pia na kumfuta kazi kocha Thomas Tuchel na kumleta Muingereza Graham Potter.

Wadhifa wa msimamizi wa kusajili vipaji vipya Chelsea ulikuwa umeshikiliwa na Marina Granovskaia pamoja na golikipa lejendari Peter Cech ambao wote walitangaza kuondoka pindi tu uongozi mpya ulipochukua hatamu kama wamiliki wa Chelsea.

Jarida la Telegraph linaripoti kuwa Boehly amejiuzulu wadhifa huo lakini ana Imani kubwa kwa kocha Potter kuendelea kuinoa Chelsea licha ya msururu wa matokeo mabaya katika siku za hivi karibuni tangu Ligi ya premia kurejelewa kufuatia likizo fupi ya kombe la dunia.

Jarida hilo liliripoti kuwa hatua ya kuachia uongozi katika kitengo cha kusajili wachezaji kunakuja baada ya kuajiri timu mpya ya kusajili, ambao baadhi yao wameanza kazi katika dirisha la uhamisho la mwezi huu.

“Wakati Boehly bado atashiriki katika matumizi ya fedha za Chelsea, Mmarekani huyo na mmiliki mwenza wake Behdad Eghbali wamekabidhi sehemu kubwa ya jukumu la uhamisho wa Chelsea kwa mkurugenzi mpya wa ufundi Christopher Vivell na Paul Winstanley, ambaye aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa kusaka vipaji duniani na kufanya Uhamisho,” Telegraph walisema.