FKF yanyima AFC Leopards kibali cha ku'stream mechi yao na Police FC mitandaoni

FKF walisema watatoa kibali tu iwapo AFC itatoa hakikisho la kutotumia mechi hiyo kujinufaisha kibiashara.

Muhtasari

• Mechi hiyo ya ligi kuu ya Kenya baina ya AFC na Police inatarajiwa kuandaliwa jioni ya Jumatano January 25 katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.

Shirikisho la FKF limekataa kutoa kibali kwa AFC kupeperusha mechi yao na Police FC mitandaoni
Shirikisho la FKF limekataa kutoa kibali kwa AFC kupeperusha mechi yao na Police FC mitandaoni
Image: Facebook//AFC Leopards

Shirikisho la soka nchini FKF limekataa ombi la timu ya AFC Leopards kutaka kupeperusha moja kwa moja mechi baina yao na timu ya Police FC kupitia mitandao yao ya kijamii.

Katika barua ambayo imetolewa Jumatano alasiri na shirikisho hilo kujibu ombi la AFC walilotuma Jumanne January 24, FKF wamekataa kutoa kibali hicho huku wakisisitiza kuwa kibali hicho kitatolewa tu iwapo lengo lake ni kuburudisha tu na wala si kusukuma masuala ya kibiashara.

“Kuhusu ombi lenu na kama tulivyotooa taarifa awali, shirikisho la FKF huwa linatoa kibali cha kupeperusha mechi mubashara mitandaoni pekee wakati ni suala la kuburudisha umma na wala si kupaisha masuala ya kibiashara. Kutokana na hilo tunajuta kuwataarifu kuwa ombi lenu la kupeperusha mechi kati ya AFC na Police FC litakubaliwa ikiwa tu shirikisho litapata hakikisho kwa njia ya maandishi kutoka kwa AFC kuwa hamtatumia matangazo hayo kujinufaisha kibiashara,” sehemu ya barua ya FKF ilisoma.

Mechi hiyo ya ligi kuu ya Kenya baina ya AFC na Police inatarajiwa kuandaliwa jioni ya Jumatano January 25 katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.

Shirikisho la FKF lilitoa onyo kuwa lina haki kisheria kutoa kibali cha mechi za ligi kuu ya humu nchini kupeperushwa iwe kwenye runinga ya kituo cha habari au kwenye mitandao ya kijamii.