"Damu yangu ni samawati" Mourinho aikataa Man-U na badala yake kuchagua Chelsea

Mreno huyo akiwa Chelsea katika vipindi viwili tofauti, aliwasaidia kushinda EPL kwa mara tatu.

Muhtasari

• “Bila shaka, muunganisho wangu Uingereza ni Chelsea, hivyo ndivyo ninavyoona mambo" - Mourinho alisema.

• Jose Mourinho sasa ni kocha wa AS Roma na amenukuliwa akisema analenga kurejea Chelsea kwa mara ya tatu.

Mourinhio aichagua Chelsea na si Man United
Mourinhio aichagua Chelsea na si Man United
Image: Talk Chelsea

Meneja wa sasa wa AS Roma ya Italia Mreno Jose Mourinho amefichua kwa mara ya kwanza ni timu gani ambayo anaishambikia katika ligi kuu ya Uingereza.

Mourinho ambaye katika ligi ya Premia amefunza timu za Chelsea, Manchester United na Tottenham Hotsupers alizungumza na jarida la The Sun ambapo alifichua timu pendwa kwenye ligi hiyo inayoshabikiwa pakubwa kote duniani.

Mourinho aliweka wazi kwamba yakija ni masuala ya EPL, bila shaka ukichukua kiwembe na kumkata, damu yake inatoka ya samawati – akiwa na maana kwamba jicho lake katika ligi hiyo hutua pale Stamford Bridge kwa Chelsea.

Itakumbukwa mreno huyo alipata mafanikio yake makubwa akiwa na Chelsea kuliko timu hizo zingine mbili katika muda wake kama kocha Uingereza.

Aliifunza Chelsea kwa mara ya kwanza kati ya mwaka 2004-07 na kuwasaidia kutua ubingwa na premia, na ujio wake tena mwaka 2013 kulimpa jina ‘The Special One’ ambapo pia alishinda nao ubingwa wa Premia kabla ya kufutwa kazi mwaka 2015.

Kocha huyo Mreno alikaa kwa muda wa miaka sita tu Stamford Bridge katika vipindi viwili vya ukocha, ambapo alishinda mataji matatu ya Premia na mataji manane. Mourinho alikua shujaa wa ibada huko Blues lakini uhusiano wake na kilabu na mashabiki wake ukawa mgumu baada ya kuhama kwake.

“Bila shaka, muunganisho wangu Uingereza ni Chelsea, hivyo ndivyo ninavyoona mambo, kama mkufunzi wa Chelsea baada ya vipindi viwili vya Chelsea na miaka sita,” Mourinho aliiambia BT Sport.

Alipoingia katika klabu hiyo ya London mwaka 2004, Mreno huyo alisaini majina makubwa ambayo yalikuja kutamba kwenye soka na kuipa Chelsea jina kubwa kote Ulaya.

Baadhi ya wachezaji aliowasaini ni kama Didier Drogba, Arjen Robben, Petr Cech miongoni mwa wengine.

Hivi karibuni, mreno huyo amenukuliwa akisema kuwa angependa kurejea tena nchini Uingereza kama kocha huku akilenga kurudi Chelsea kwa mara ya tatu, huku timu hiyo ikiendelea kuandikisha matokeo mabaya chini ya uongozi wa kocha Graham Potter.