Jalang’o ataka Ligi ya Soka ya Kenya kuwa baina ya makaunti

Mbunge huyo amesema magavana watawekeza sana katika mchezo huo na kuboresha vifaa katika kaunti zao.

Muhtasari

•Jalang'o alishiriki wazo la kubadilisha Ligi ya Soka ya Kenya kuwa baina ya kaunti mbalimbali na waziri wa Michezo, Ababu Namwamba.

•Jalang'o alibainisha kuwa katika ligi zilizoendelea zaidi duniani kama vile EPL nchini Uingereza, timu zote zinawakilisha miji fulani

wakati wa mchuano wa Gor Mahia dhidi ya AFC katika uwanja wa Nyayo, mnamo Januari 29, 2023.
Mbunge Phelix Odiwuor almaarufu Jalang'o na Waziri wa Michezo Ababu Namwamba wakati wa mchuano wa Gor Mahia dhidi ya AFC katika uwanja wa Nyayo, mnamo Januari 29, 2023.
Image: INSTAGRAM// JALANG'O

Mbunge wa Lang'ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang'o ametoa pendekezo maalum la kufufua mchezo wa kandanda nchini Kenya.

Siku ya Jumatatu, mbunge huyo wa muhula wa kwanza alifichua kwamba alishiriki wazo la kubadilisha Ligi ya Soka ya Kenya kuwa baina ya kaunti mbalimbali na waziri wa Michezo, Ababu Namwamba.

Jalang’o alipendekeza kaunti 20 ambazo zitaibuka bora zaidi katika hatua ya mchujo kucheza katika Daraja la Kwanza huku kaunti zingine 20 zinazofuata zikicheza katika Daraja la Pili. Kaunti saba za mwisho zitashiriki katika Divisheni ya Tatu ya ligi iwapo pendekezo hilo litatekelezwa.

"Ligi gani! Unaweza kufikiria debi!! Kaunti ya Nyeri inapokutana na kaunti ya Muranga! Je, unaweza kufikiria debi ya Garissa-Marsabit? Au Kisumu-Homabay? Au Siaya-Nyeri? Au Kisii-Nyamira, Matoke Derby! Baringo Vs Uasin Gishu? Kilifi Mombasa derby?" alisema kwenye mtandao wa Instagram.

Mbunge huyo aliteta kuwa huku kaunti tofauti zikishindana, magavana watawekeza sana katika mchezo huo na kuboresha vifaa katika kaunti zao.

Pia aliteta kuwa itawapa wachezaji wenye talanta ambazo hazijatambuliwa jukwaa la kuonyesha taifa na dunia kile wanachoweza kufanya. 

"Mvulana kutoka Turkana atasafiri lini kwenda Nyamira? Je, unaweza kufikiria debi ya Jiji? Nairobi vs Kisumu? Tharaka Nithi dhidi ya Kaunti ya Meru? Miraa Derby! Muthokoi Derby! Machakos vs Kitui! Hakuna gavana ambaye angetaka timu yake icheze kwenye uwanja chakavu!" alisema mbunge huyo.

Jalang'o alibainisha kuwa katika ligi zilizoendelea zaidi duniani kama vile EPL nchini Uingereza, timu zote zinawakilisha miji fulani, jambo ambalo linapatia timu mashabiki wa wazi kutoka mji wa nyumbani.

Hivyo, Alitaka waziri Namwamba kuiga EPL na kuwa na kila klabu katika Ligi Kuu ya Kenya kuwakilisha kaunti.

"Mchuano wa Gor Mahia na AFC ndio pekee katika KPL unaovutia watu wengi na umati unaendelea kupungua na hatuwezi kustahimili hata kulipa wachezaji! Ninaweka dau kuwa huwezi hata kutaja timu 10 katika KPL! Je, unajua sofapaka wamerejea kwenye ligi?" alihoji na kutaka hilo kutupiliwa mbali.

Kwa sasa, Ligi Kuu ya Kenya ina vilabu 18 vilivyo chini ya usimamizi tofauti. Gor Mahia, AFC Leopards, Tusker na Sofapaka zimetawala ligi hiyo kwa muda mrefu.