Tulikusanya zaidi ya Ksh 3M kutoka kwa debi ya Mashemeji - AFC Leopards

Tikiti za kawaida za Ksh 300 zilinunuliwa na watu 9565 huku zile za VIP za Ksh 1000 zikinunuliwa na watu 461.

Muhtasari

• Leopards walikuwa wenyeji wa mechi hiyo na walisema ndio ilikuwa mechi ya kwanza ya msimu kuuza tikiti nyingi.

Mashabiki wa AFC Leopards wakisherehekea baada ya mechi
Mashabiki wa AFC Leopards wakisherehekea baada ya mechi
Image: AFC LEOPARDS//FACEBOOK

Klabu ya AFC Leopards ambao ndio walikuwa wenyeji katika mechi ya Mashemeji iliyofanyika wikendi iliyopita ugani Nyayo Nairobi imetangaza kutengeneza pesa nyingi kutokana na mechi hiyo.

Kupitia taarifa ambayo Leopards walichapisha mitandaoni, walisema kuwa mechi hiyo iliandikisha historia kama moja ambayo ilipata mafanikio makubwa, mashabiki wengi wakijitokeza kuhudhuria katika miaka ya hivi karibuni.

Leopards ilisema ilitengeneza shilingi milioni 3.3 kutoka kwa viingilio ambapo tikiti za kawaida za shilingi 300 zilinunuliwa na mashabiki 9,565 huku zile za sehemu maalum almaarufu VIP ambazo zilikuwa zinauzwa kwa shilingi elfu moja zikinunuliwa na watu 461.

Leopards waliwashukuru mashabiki na washikadau wa soka nchini kwa kujitokeza kwa wingi na kuhudhuria mechi hiyo, huku wakisema ni ishara nzuri ya kuonesha mafanikio makubwa katika soka la Kenya ambalo limefifia katika miaka michache iliyopita.

“Zaidi ya tikiti 10,000 ziliuzwa kwa wikendi ya #MashemejiDerby, na kuifanya kuwa mechi yetu iliyohudhuriwa na watu wengi zaidi kwenye ligi msimu huu hadi sasa. Tiketi 461 kati ya hizo zilikuwa za sehemu ya VIP na 9565 zilikuwa za matuta. Kwa mara nyingine tena asante kwa kujitokeza na kufanya mechi kuwa hai,” AFC Leopards walitoa taarifa.

Mechi hiyo iliisha kwa sare kappa huku Leopards wakisalia katika nafasi ya 8 kwa alama 18 na Gor Mahia wakipanda hadi nafasi ya pili kwa alama 24 nyuma ya viongozi Nzoia Sugar wenye alama 27.