Aguero apiga bomu Arsenal, asema EPL itaenda Manchester United au City

Aguero alisema ni mapema sana watu kuanza kusema Arsenal ndio mabingwa watarajiwa.

Muhtasari

Arsenal haijashinda Ligi ya Premia tangu wahamie kwenye Uwanja wa Emirates mwaka 2006.

Aliyekuwa mshambuliaji matata wa timu ya Manchester City, Muargentina Sergio Kun Aguero ametoa tamko ambalo litachefua mioyo ya mashabiki wengi wa timu ya Arsenal.

Japo Arsenal mpaka sasa wameshikilia usukani kileleni mwa jedwali la ligi kuu ya premia Uingereza kwa alama zaidi ya tano baada ya mechi za mzunguko wa 19, Aguero bado anahisi kuwa hawafai kupewa nafasi moja kwa moja kuwa ndio mabingwa watarajiwa.

Aguero anahisi kuwa bado ni mapema sana kwa mtu yeyote kuanza kuweka matumaini yake kuwa Arsenal ndio mabingwa wa mwaka huu, huku akisema kuwa timu kama Manchester City, United na Newcastle wapo na nafasi kubwa ya kushinda taji hilo mbele ya Arsenal.

“Kwa jinsi mambo yalivyo, itaenda kwa Arsenal, City au United," gwiji huyo wa City Aguero aliambia Stake.com. "Newcastle pia haiwezi kupunguzwa. Walicheza kipindi kizuri cha kwanza cha michuano hiyo.”

Vijana wa Mikel Arteta kwa sasa wako kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 50 na wana faida ya pointi tano zaidi ya Manchester City inayoshika nafasi ya pili. Arsenal wamepoteza mara moja pekee kwenye ligi ya ndani katika mechi 19 walizocheza, huku kichapo chao pekee kikiwa cha mwezi Septemba mikononi mwa wapinzani, Man United.

Arsenal haijashinda Ligi ya Premia tangu wahamie kwenye Uwanja wa Emirates mwaka 2006, huku mataji yao matatu yote yakiibuka wakicheza kwenye uwanja wao wa zamani wa Highbury.