Kocha wa AFC Leopards ajipata pabaya kwa kuita mwanahabari 'mjinga'

Aussems aliyejawa na hamaki baada ya sare kapa dhidi ya Nzoia alimfokea mwandishi wa habari za michezo.

Muhtasari

• "Pia tutampa fursa ya kueleza upande wake wa hadithi," alithibitisha Otieno., mtendaji mkuu wa FKF.

Kocha wa AFC Leopards, Patrick Aussems.
Kocha wa AFC Leopards, Patrick Aussems.
Image: Facebook,

Shirikisho la soka nchini FKF limedhibitisha kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu video moja inayosambaa mitandaoni ikimuonesha kocha wa AFC Leopards, Mbelgiji Patrick Aussems akimuita mwanahabari ‘mjinga’.

Kocha Aussems alikuwa na mkutano na wanahabari baada ya kukamilika kwa mechi yao dhidi ya viongozi wa ligi Nzoia Sugar iliyokamilika kwa sare kapa.

Mtendaji Mkuu wa FKF Barry Otieno alisema kisa hicho kitatumwa kwa Kamati ya Nidhamu. "Pia tutampa fursa ya kueleza upande wake wa hadithi," alithibitisha Otieno.

Siku ya Jumapili, Aussems alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari alisema, "Wewe, wewe ni mjinga rafiki yangu," na akarudia maneno halisi.

Inaeleweka kwamba mwandishi huyo wa habari za michezo alimuuliza Aussems swali la kuhusu ni kwa nini hakuweza kuondoka uwanjani hata baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu – swali ambalo lilimkera Aussems ambaye si yeye alioneshwa kadi nyekundu bali ni kocha wa makipa wa Ingwe.

Na hapo ndipo alimtemea maneno hayo makali ya kumdunisha huku akitaka kubaini kitambulisho chake ili asije akajibu swali linguine kutoka kwake kwani ni ‘mjinga’

"Ni Webo aliyepokea kadi nyekundu sio mimi. Wewe ni mpumbavu. Kwa kweli, wacha nione jina lako… tafadhali usiniulize swali lingine lolote,” aliongeza Aussems.

Aussems ambaye alionekana kutofurahia matokeo ya mechi hiyo iliyochezwa kaunti ya Bungoma alisema kuwa marefa walikuwa wanaegemea upande mmoja na kuonea timu yake.

Mbellgiji huyo amekuwa kwenye hatamu kama kocha wa AFC Leopards kwa mwaka mmoja na nusu uliopita ila hajafanikiwa kushinda taji lolote na miamba hao wa soka la Kenya.