Leeds United wamtimua kocha Jesse Marsch kabla ya kumenyana na Man United

Klabu hiyo imemtimua Marsch mwaka mmoja tu baada ya kumteua.

Muhtasari

•Marsch alijiunga na klabu hiyo ya EPL mwezi Machi mwaka jana baada ya kutimuliwa kwa aliyekuwa kocha, Marcelo Bielsa.

•Klabu hiyo ambayo kwa sasa iko katika nafasi ya 17 pia iliwatimua wasaidizi wa Marsch; Rene Maric, Cameron Toshack na Pierre Barrieu.

Jesse Marsch
Image: HISANI

Leeds United wamempiga kalamu kocha wao mkuu Jesse Alan Marsch , takriban mwaka mmoja baada ya kumteua.

Marsch alijiunga na klabu hiyo ya EPL mwezi Machi mwaka jana baada ya kutimuliwa kwa aliyekuwa kocha, Marcelo Bielsa.

Mmarekani huyo klabu mwenye umri wa miaka 49 alisaidia Leeds United kumaliza msimu uliopita wa 2021/22 katika nafasi ya 17 kwa pointi 38 na hivyo kusalia kwenye ligi kuu. Hata hivyo, amekuwa akiandikisha matokeo hafifu katika mechi ya hivi majuzi na hivyo kupelekea kutimuliwa kwake siku ya Jumatatu.

"Tungependa kumshukuru Jesse na kikosi chake cha nyuma kwa juhudi zao na tunawatakia heri kwa siku zijazo," Leeds United ilisema katika taarifa.

Klabu hiyo ambayo kwa sasa iko katika nafasi ya 17 pia iliwatimua wasaidizi wa Marsch; Rene Maric, Cameron Toshack na Pierre Barrieu.

Mchakato wa kumtafuta na kumteua kocha mpya bado unaendelea  huku mashabiki wa klabu hiyo wakiombwa kuwa na subira.

Huku wakitarajiwa kumenyana na Manchester United siku ya Jumatano, usimamizi wa klabu hiyo umetangaza kwamba Michael Skubala, Paco Gallardo na Chris Armas ndio wataongoza wachezaji kwenye mchuano huo.

Klabu hiyo itakuwa inatafuta ushindi wa kwanza tangu November 5, 2022 watakaposafiri hadi Old Trafford usiku wa Jumatano.