"Nawapenda zaidi leo kuliko jana" - Arteta aliwafariji vijana wake kwa kupigwa na Eveton

Gunners walipokezwa kipigo chao cha kwanza cha msimu mnamo Septemba mwaka jana na Red Devils.

Muhtasari

• Arsenal bado wamesalia kileleni mwa jedwali kwa alama 50, tano zaidi ya namba 2 Manchester City.

Mikel Arteta wa Arsenal
Mikel Arteta wa Arsenal
Image: GETTY IMAGES

Wikendi iliyopita, viongozi wa jedwali la ligi kuu Uingera EPL Arsenal walichakazwa baada ya kupokezwa kipigo chao cha pili msimu huu mikononi mwa timu ya mkiani, Everton.

Kipigo cha Arsenal cha kwanza msimu huu kilijiri mwaka jana mikononi mwa watani wao wa jadi, Manchester United na tangu hapo kabla ya kukutana na shoka la Everton, vijana wa kocha Mikel Arteta walikuwa na msururu wa matokeo mazuri, wakijinafasi vizuri kulinyakua taji la ligi ya Premia kwa mara ya kwanza katika miaka mingi.

Kipigo mikononi mwa Everton kilikuwa cha kushangaza na kuwapiga butwaa vijana wa Arteta kwani hawakuwa wanadhani kabisa timu ya mkiani inayopambana udi na ambary kujinasua kutoka eneo hatari la kushushwa daraja ingewachakaza.

Sasa imebainika kuwa kocha Arteta hata baada ya kipigo hicho cha kudhalilisha, hakuwakoromea wachezaji wake bali aliwatia moyo kwa maneno ya kufariji akiwahakikishia upendo wake hata baada ya kudhalilishwa na timu ya mkiani.

“Niliwaambia wachezaji ninawapenda zaidi sasa kuliko nilivyofanya wiki iliyopita na mwezi uliopita.”

Arteta atatumai kupata matokeo mengine chanya kutoka kwa wachezaji wake wanapojiandaa kukabiliana na Brentford kwa mara nyingine katika mechi yao ya marudiano kwenye Uwanja wa Emirates mnamo Februari 11.

Mhispania huyo amesisitiza jinsi anavyojaribu kudumisha hali nzuri ya kiakili na hali nzuri miongoni mwa kikosi na huku kukiwa na uchambuzi wa jinsi Everton walivyobatilisha safu ya mashambulizi ya Arsenal, Arteta hatazingatia kichapo hicho na badala yake atatafuta kurejea katika njia za ushindi wikendi.