Timu za EPL zaungana kutaka Manchester City kufukuzwa kutoka ligi ya Premia

Timu kubwa zikiwemo Arsenal, Chelsea, Man United, Liverpool, Tottenham wanahisi kufukuzwa kwa City ndio suluhu.

Muhtasari

• City wanakabiliwa na msururu wa mashtaka zaidi ya 100 kuhusu ukiukaji wa kanuni za matumizi ya fedha kati ya mwaka 2009-2018.

Timu za EPL zafunga macho ya huruma dhidi ya Man City
Timu za EPL zafunga macho ya huruma dhidi ya Man City
Image: Twitter

Zogo na sakata linaloizunguka timu ya Manchester City linazidi kukolea na kuelekea pabaya kila sekunde iendayo kwa Mungu huku sasa taarifa zikiibuka kuwa timu zingine katika ligi kuu ya Preia zinasukuma kutaka City ifukuzwe kutoka kushiriki ligi hiyo.

Kulingana na kituo cha habari cha Sky Sports, timu nyingine za Premia zinahisi kwamba City kupokonywa pointi tu na kupewa adhabu ya kunyanganywa mataji ambayo walishinda katika kipindi husika cha sakata hilo si adhabu tosha, huku wakisukuma sasa timu hiyo kufungiwa kabisa kutoshiriki ligi ya EPL.

Jambo la kufurahisha ni kwamba ripoti hiyo inaeleza zaidi kwamba klabu ambazo zinapigania hatua kali zaidi ni zile zinazojulikana kama 'Sita Bora' - Manchester United, Chelsea, Arsenal, Tottenham Hotspur na Liverpool.

Ligi ya Premia imeishtaki Man City kwa zaidi ya makosa 100 ya ukiukaji wa kanuni za fedha. Kesi hiyo imekabidhiwa kwa tume huru, ambayo sasa imepangwa kubaini uhalali wa mashtaka na kuchukua hatua zinazohitajika.

Bodi ya ligi ilitangaza Jumatatu, Februari 6, kwamba Wananchi walikuwa wakikabiliwa na zaidi ya ukiukwaji 100 wa sheria za kifedha. Matukio ya hivi punde kwenye Uwanja wa Etihad yanaonekana kuathiri hali ya klabu, huku Guardiola akionekana mtu aliyehuzunika wakati wa mazoezi.

Awali, Radio Jambo pia iliripoti juu ya mwanachama wa Arsenal kuteuliwa kuwa mkuu wa tume huru inayochunguza mashtaka dhidi ya Man City. Murray Rosen KC, ambaye anajiorodhesha kama shabiki wa Arsenal katika wasifu wake, sasa anatazamiwa kuongoza tume ambayo itaamua ikiwa mabingwa hao watetezi wana hatia. Wakili huyo ndiye mwenyekiti wa jopo la mahakama la EPL na atatarajiwa kuunda timu ya watu watatu kusikiliza maoni kutoka pande zote mbili.