(+video) Maelfu ya Nzige wavamia uwanja Ronaldo akiweka rekodi ya mabao 500

Ronaldo alifunga mabao 4 dhidi ya Al Wehda na kuweka rekodi ya mabao 500 kwa klabu, akivitumikia vilabu 5 tofauti mpaka sasa.

Muhtasari

• Ronaldo alifungua vitabu vya mabao yake matatu kwa mech moja maarufu Hattrick ya kwanza katika ligi ya Saudia usiku wa Alhamisi.

• Al Nassr ilishinda kwa mabao 4 kapa, yote ambayo yalifungwa na mchezaji huyo wa Ureno mwenye miaka 38.

Christiano Ronaldo si mgeni katika masuala ya kuvunja na kuandikisha rekodi mpya.

Mchezaji huyo usiku wa Alhamisi alikuwa nguzo muhimu katika ushindi wa timu yake ya Al Nassr ilipokuwa ikicheza ugenini dhidi ya Al Wehda kwenye ligi kuu ya Saudia.

Al Nassr ilishinda mechi hiyo kwa mabao manne kappa, mabao yote ambayo yalitiwa wavuni na Christiano Ronaldo na hivyo kuweka rekodi mpya ya kuwa mchezaji mwenye mabao Zaidi ya 500 kwa kutumikia vilabu tu.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno, ambaye alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya miaka 38 Jumapili, hakuwa na kipingamizi dhidi ya wenyeji Al Wehda, akifunga mara nne ndani ya dakika 30 na kuiongoza timu yake kushinda 4-0.

Baada ya mabao hayo 4, Ronaldo sasa amefunga mabao 503 ya ligi kwa vilabu vitano katika ligi tano tofauti za ligi kuu. Alishinda 103 kwa Manchester United, 311 kwa Real Madrid, 81 kwa Juventus, tatu kwa Sporting Lisbon, na sasa ana tano akitumikia uzi wa Al Nassr.

Mshindi huyo mara tano wa Ballon D’Or alisaini mkataba wa miaka miwili na nusu na Al Nassr mwezi Desemba, ulioripotiwa kuwa na thamani ya zaidi ya £177m, na aliteuliwa kuwa nahodha wa timu hiyo.

Hata hivyo mechi hiyo ilikuwa ya aina yake baada ya nzige wengi ajabu kuonekana kuvamia uwanja huo Ronaldo akiweka rekodi ya mabao.

Katika video na picha ambazo zimeonekana kwenye mitandao ya kijamii, mashabiki walivamiwa na nzige mpaka wakaacha viti vyao, wengine wakisimama kushuhudia mechi huku wamejifunika vichwa na nzige wakitanda juu ya viti.

 

Al Nassr wanaongoza jedwali baada ya michezo 16, sawa na pointi 37 na Al Shabab walio nafasi ya pili.