Timu ya mpira wa miguu ya Shabana kutoka eneo pana la Gusii inaomboleza kifo cha mwenyekiti wao mheshimiwa Dkt Nyandoro Kambi.
Timu hiyo ambayo inashikilia nafasi ya kwanza kwenye jedwali la ligi kuu ya National Super League, NSL ilitangaza habari hizo za tanzia usiku wa kuamkia Jumamosi kupitia kurasa za mitandao yao ya kijamii na kusema kwamba Kambi mpaka kifo chake alikuwa ndiye mwenyekiti wao.
Shabana walimuomboleza wakili Kambi kama mwenyekiti aliyefanya majukumu yake kwa moyo wa kujitolea, na jitihada zake ndizo zilihakikisha mibabe hao wa soka ya wanaume Gusii wanapata nafasi ya kukwea kutoka ngazi za chini hadi kuingia kwenye ligi ya NSL ambaye ni ligi ya pili kwa ukubwa baada ya ligi kuu ya FKF PL.
“Tunasikitika kukuthibitishia kuondokewa na Mwenyekiti wa klabu yetu, Mhe. Dk. Nyandoro Kambi LLB, ambaye hadi wakati wa kifo chake alikuwa Mwenyekiti wa klabu yetu pendwa, Shabana FC. Alikuwa shabiki aliyejitolea na kila mara alikuwa amejitolea kuhakikisha kuwa klabu hiyo inapanda daraja hadi Ligi Kuu ya Kenya. Utabaki milele mioyoni mwetu Daktari,” taarifa hiyo ya Tanzia ilisoma.
Chini ya Uongozi wa Shabana kama mwenyekiti, Kambi alihakikisha maslahi ya wachezaji wa timu hiyo yanashughulikiwa kikamilifu na kuwapa motisha wa kuanza msimu wa mwaka huu kwa fujo ya aina yake ambapo mpaka sasa baada ya mzunguko wa 10, Shabana inashikilia nafasi ya kwanza kwenye jedwali la NSL kwa alama 25.
Jumatano wiki hii, Shabana walipoteza mechi yao ya kwanza ya msimu dhidi ya Kibera Blalck Stars jijini Nairobi lakini bado wanasalia kileleni, huku Kibera wakiwa nafasi ya pili kwa mbali na pointi 20.
Makiwa kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wapenzi wote wa soka nchini!