CEO wa Brighton: Nimeambia wafanyikazi wa usafi kuwa macho, Chelsea inaweza wasajili

Aliyasema haya baada ya uvumi kuwa Chelsea inalenga kuchukua kocha wao De Zerbi, baada ya kuchukua Potter.

Muhtasari

• Afisa mkuu mtendaji huyo alisema ametoa tahadhari kwa kila mtu katika timu yake kuwa macho kwani Chelsea wanataka kuchukua kila mtu.

CEO wa Brighton aiponda Chelsea
CEO wa Brighton aiponda Chelsea
Image: Facebook

Siku mbili zilizopita, kuliibuka uvumi mkali kwenye mitandao ya kijamii kwa timu ya Chelsea kwa mara nyingine tena ilikuwa inapanga njama ya kuwapokonya Brighton & Hoven kocha wao, Muitaliano Roberto De Zerbi.

Itakumbukwa kwamba miezi michache iliyopita, De Zerbi aliteuliwa kama kocha mpya wa Brighton baada ya Chelsea kuwapokonya Brighton kocha wao Muingereza Graham Potter ambaye rekodi yake katika klabu hiyo la London haijakuwa nzuri tangu kumalizika kwa mechi za kombe la dunia nchini Qatar.

Baada ya uvumi wa uvamizi wa Chelsea katika kambi ya Brighton tena, Afisa Mkuu Mtendaji wa timu hiyo amezungumza na kuonekana kutupa makombo kwa Chelsea kwa njia ya kejeli.

Paul Barber alisema kwa kejeli kwamba huwa anapenda sana kuzipokea simu kutoka kwa uongozi wa timu ya Chelsea wakati wanazungumzia mambo tofauti lakini ikifika ni maswala la simu ya kuomba huduma za kocha wao, hapo ndipo anachora mstari mkubwa wa kujitenga na simu za Chelsea.

"Nina furaha kuchukua simu kwa Chelsea ... mbali na wakati ni kwa ajili ya makocha wetu," Barber aliiambia FTLive, kulingana na mwanahabari wa habari za spoti, Fabrizio Romano.

Barber pia alizamisha mkuki wa kejeli kwenye nyoyo za mashabiki wa wapenzi wa Chelsea akisema kwamba hata ameshatoa tahadhari kwa wafanyikazi wa usafi katika timu hiyo kuwa macho kwani Chelsea wanaweza wasajili wakati wowote bila habari yake.

"Nimewaambia wafanyikazi wa usafi kuwa waangalifu, wanaweza kuwindwa pia," Paul Barber aliongeza.

Muda mchache baada ya Chelsea kuipokonya Brighton kocha Potter, walirudi tena kwa kishindo ambapo walimwinda msimamizi wa soko la uhamisho wa wachezaji wa timu hiyo Paul Winstanley ambaye alimfuata Potter kwenda Chelsea.