Wachezaji 2 wa Chelsea wapigana uwanjani wakati wa sare dhidi ya Everton (Video)

Beki Kalidou Koulibaly na nahodha Mateo Kovacic walikabiliana vikali kunako dakika ya 61 Chelsea wakijiandaa kucheza mpira wa kona.

Muhtasari

• Haikubainika wawili hao walikuwa wananyoosheana vidole kwa nini lakini kocha Potter ana kazi pevu ya kutuliza kambi yake.

Ufa mkubwa unazidi kukisiwa kuikumba kambi ya timu ya Chelsea, huku timu hiyo ikiendeleza rekodi mbovu katika ligi ambayo mpaka sasa imewaweka katika nafasi ya kumi kwenye jedwali.

Jumamosi usiku wakati wa mechi ya ligi kuu ya premia dhidi ya Everton, wachezaji wawili wa timu hiyo walionekana wakipapurana vikali kwa maneno na kunyoosheana vidole uwanjani.

Kiungo Mateo Kovacic na beki Kalidou Koulibaly walionekana kutupiana maneno makali mpaka nusra kumenyana kimwili kabla ya beki Weslay Fofana kufika kwa haraka na kutuliza hali hiyo.

Katika mechi hiyo, Chelsea walikuwa wameongoza lakini bao la dakika za mwisho kutoka kwa Everton lililazimisha sare ya kufungana mabao mawili kwa mawili na Chelsea kupoteza nafasi ya kuongeza pointi na angalau kupanda kwenye jedwali hilo lenye ushindani mkali.

Joao Felix alifunga bao lake la pili katika rangi za Chelsea kabla ya Abdoulaye Doucore kurejesha usawa kwa kichwa kizuri kilichopigwa nyuma ya kipa Kepa Arrizabalaga. Kai Havertz alidhani ameshinda mchezo wa Chelsea kwa penalti dakika ya 76, lakini Simms alitoka benchi na kufunga bao lake la kwanza la ligi ya premia.

Wakati Chelsea wakijiandaa kupiga kona katika dakika ya 61, Kovacic na Koulibaly walionekana kurushiana maneno makali, huku wenzao wakiingia haraka ili kutuliza mvutano huo. Haijabainika suala la wawili hao lilikuwa ni nini.

Kovacic alikuwa nahodha wa siku hiyo, kwani amekuwa kwenye mechi tatu zilizopita, huku Cesar Azpilicueta na Thiago Silva wakiendelea kukosekana.