Mesut Ozil astaafu soka, afichua sababu zake

Ozil alisema imekuwa safari nzuri iliyojaa nyakati na hisia zisizoweza kusahaulika.

Muhtasari

•Kiungo wa kati Mesut Ozil ametangaza kustaafu kwake baada ya taaluma ya kucheza soka ya takriban miaka 17.

•Alishukuru vilabu vyake vya zamani vikiwemo Shalke 04. Werder Bremen, Real Madrid, Arsenal, Fenerbahce na Basaksehir.

Image: HISANI

Kiungo wa kati Mesut Ozil ametangaza kustaafu kwake baada ya taaluma ya kucheza soka ya takriban miaka 17.

Katika taarifa yake siku ya Jumatano, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 alisema kuwa ameridhishwa na safari yake ya kucheza kandanda na kutoa shukrani za dhati kwa nafasi zote ambazo alipata kucheza.

Ozil ambaye hivi majuzi amekuwa akichezea klabu ya Uturuki, Istanbul Basaksehir alidokeza kuwa majeraha yamemlazimu kutundika buti zake.

"Nimekuwa na bahati ya kuwa mchezaji wa soka wa kulipwa kwa takriban miaka 17 sasa na ninahisi kushukuru sana kwa nafasi hiyo. Lakini katika wiki na miezi ya hivi majuzi, na kuwa pia nimepata majeraha, imekuwa wazi zaidi na zaidi kuwa ni wakati wa kuondoka kwenye jukwaa kubwa la soka,” alisema.

Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani alisema imekuwa safari nzuri iliyojaa nyakati na hisia zisizoweza kusahaulika.

Alitoa shukrani kwa vilabu vyake vya zamani vikiwemo Shalke 04. Werder Bremen, Real Madrid, Arsenal, Fenerbahce na Basaksehir. Pia aliwashukuru wachezaji wenzake katika vilabu hivyo vyote na makocha ambao walimfunza.

"Shukrani za kipekee lazima ziende kwa familia yangu na marafiki zangu wa karibu. Wamekuwa sehemu ya safari yangu kutoka siku ya kwanza na wamenipa upendo na msaada mkubwa, kupitia nyakati nzuri na mbaya," alisema.

Kiungo huyo wa kati pia aliwashukuru mashabiki wake kwa upendo ambao wamemwonyesha katika safari yake ya soka.

Aidha, alidokeza kwamba anapanga kujikita katika kutumia wakati mwingi zaidi na familia yake ndogo.

"Sasa natazamia kila kitu kilicho mbele yangu na mke wangu mzuri, Amine, na binti zangu wawili warembo, Eda na Ela- lakini mnaweza kuwa na uhakika kwamba mtanisikia mara kwa mara kwenye chaneli zangu za mitandao ya kijamii,” aliandika

Mashabiki wake kote duniani wameendelea kumpongeza na kumtakia kila la kheri katika hatua yake ijayo.