Wanabunduki waghadhabika baada ya mchezaji wa Man City kumchezea vibaya Odegaard

Mashabiki wa Arsenal wamesema ni njama ya Man City kuwazuia kunyanyua Kombe la EPL.

Muhtasari

•Martin Odegaard  alijaribu kufunga akiwa ndani ya sanduku la Uhispania ila shuti lake likazuiwa na Rodri.

•Odegaard, ambaye alikamilisha dakika zote 90 uwanjani, hata hivyo hakuonekana kupata jeraha la aina yoyote.

akizuia shuti la Martin Odegaard usiku wa Jumamosi.
Rodri akizuia shuti la Martin Odegaard usiku wa Jumamosi.
Image: HISANI

Mashabiki wa klabu ya Arsenal wameendelea kueleza ghadhabu yao kwa kiungo wa Manchester City Rodrigo Hernández Cascante, almaarufu Rodri baada ya kumchezea vibaya nahodha wao Martin Odegaard wakati Norway ilipokuwa ikimenyana na Uhispania katika mechi ya kufuzu EURO 2024 usiku wa Jumamosi.

Norway ilipoteza 3-0 dhidi ya Uhispania kufuatia mabao mawili ya Joselu na moja la Dani Olmo katika mechi ya kwanza ya Kundi A.

Katika kipindi cha kwanza, Martin Odegaard ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Norway alijaribu kufunga akiwa ndani ya sanduku la Uhispania ila shuti lake likazuiwa na Rodri. Baada ya kuzuia shuti hilo, Rodri aliteleza kuelekea kwa miguu ya kiungo huyo wa Wanabunduki na kumwangusha chini kwa kishindo.

Kwa mshangao wa watu wengi, hakuna penalti iliyotolewa na kiungo huyo wa Manchester City hata hakuonyeshwa kadi. Mashabiki wengi wa Arsenal walihisi kuwa penati ingefaa kutolewa kwa ajili ya nahodha wao.

"Faulo mbaya kabisa kutoka kwa Rodri kwa Odegaard," shabiki wa Arsenal, Ardent Gooner alisema kwenye Twitter.

Rimedi alisema, "Tackle hilo la Rodri lilikuwa hatari. Martin Odegaard alikuwa na BAHATI ya kukwepa jeraha ambalo lingeweza kuharibu nafasi za Arsenal kutwaa ubingwa. ❌ Hakuna penati iliyotolewa 🙅🏾‍♂️,"

"Je, inakuwaje jinsi Rodri alivyokabiliana na Ødegaard sio penalti? Uhispania inahitaji kuchunguzwa kwa kumlipa Ref kama Barcelona. Arsenal bado inamhitaji kiungo huyo akiwa sawa," alisema Tierney & Saka.

Odegaard, ambaye alikamilisha dakika zote 90 uwanjani, hata hivyo hakuonekana kupata jeraha la aina yoyote.

"Nina uhakika kabisa nilipaswa kupewa penalti," aliwaambia wanahabari baada ya mechi "Alikuja na kiatu chake kwenye kifundo changu."

Aliongeza, "Lakini nina uhakika nitaadhibiwa [kama nikisema zaidi]. Sijisumbui kusema chochote kingine kuhusu refa. Ni afadhali kutosema lolote.’

Meneja wa Norway Stale Solbakken kwa upande wake alisema: "Ni penalti ya wazi! 'Alikuwa amemaliza shuti na huwezi kumchezea vibaya.

Nikimwangusha mtu chini baada ya mpira kuondoka, basi ni penalti? Napata kuchoshwa kidogo kwa hili."