Wenger na Ferguson waongezwa kwenye kitabu cha magwiji wa EPL

Wawili hao ndio mameneja wa kwanza kuingizwa kwenye Hall of Fame.

Muhtasari

•Wakati wa kipindi chake na Manchester United, Ferguson alishinda mataji 13 ya EPL huku Wenger akishind kombe hilo mara tatu.

Arsene Wenger na Sir Alex Ferguson
Image: HISANI

Siku ya Jumatano, makocha wa zamani Arsene Wenger na Sir Alex Ferguson waliongezwa kwenye kitabu cha wahusika mashuhuri wa Ligi Kuu ya Uingereza almaarufu Hall of Fame.

Wawili hao ambao walisimamia vilabu vya Arsenal na Manchester United mtawalia kwa muda mrefu walitambuliwa kwa mafanikio yao makubwa katika kipindi cha ukufunzi wao.

"Magwiji wawili waliosaidia kufafanua Ligi ya Premia, Sir Alex Ferguson na Arsene Wenger ndio wateule wawili wa kwanza wa 2023 wa PL Hall of Fame," taarifa ya Ligi Kuu ya siku ya Jumatano ilisomeka.

Ferguson na Wenger ndio mameneja wawili wa kwanza kuingizwa kwenye Hall of Fame.

Hall of Fame ilizinduliwa mwaka wa 2021 huku David Beckham, Dennis Bergkamp, ​​Eric Cantona, Thierry Henry, Roy Keane, Frank Lampard, Steven Gerrard na Alan Shearer wakiwa watu wa kwanza kutambuliwa pale.

Mwaka jana, Sergio Aguero, Didier Drogba, Vincent Kompany, Wayne Rooney, Peter Schmeichel, Paul Scholes, Patrick Vieira na Ian Wright waliongezwa

Akizungumza wakati wa kuongezwa kwenye Hall of Fame, Ferguson aliwasifia wachezaji wa zamani wa klabu hiyo ambao walichangia katika mafanikio yake na Mashetani Wekundu.

Kwa upande wake, Wenger alibainisha kwamba alijivunia sana kupata nafasi ya kuongoza klabu ya Arsenal kwa misimu 22.

"Kushinda hakutoshi. Wajibu wa ukamilifu ndio muhimu zaidi kwangu," Wenger alisema.

Baadhi ya wachezaji tajika wa zamani wa vilabu hivyo vikubwa waliwasifia makocha hao wa zamani kwa umahiri wao.

Wakati wa kipindi chake na Manchester United, Ferguson alishinda mataji 13 ya EPL huku Wenger akishind kombe hilo mara tatu.