Mtangazaji Ghost Mulee ateuliwa tena kuwa Kocha

Mtangazaji huyo ameteuliwa kama kocha wa timu ya wanawake ya Gaspo.

Muhtasari

•Ghost alitia mkataba wa muda usiobainishwa na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL) siku chache zilizopita.

•Mwenyekiti wa Gakpo, Edward Githua aliweka wazi kuwa walimteua Mulee kutokana na uzoefu wake mkubwa katika ukufunzi.

Jacob Ghost Mulee
Image: RADIO JAMBO

Aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Harambee Stars, Jacob 'Ghost' Mulee ameteuliwa kusimamia klabu ya wanawake ya Gaspo.

Ghost alitia mkataba wa muda usiobainishwa na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL) siku chache zilizopita na kuchukua nafasi ya mkufunzi  James Ombeng ambaye amekuwa kaimu kocha mkuu.

"Kwa heshima kubwa na fahari, tuna bahati ya kumtangaza JACOB 'GHOST' MULEE kama sehemu ya familia yetu kubwa. Kambi imehamasishwa sana na imejiandaa tena kwa kozi hiyo," taarifa ya klabu hiyo ilisoma.

Mwenyekiti wa Gakpo, Edward Githua aliweka wazi kuwa walimteua Mulee kutokana na uzoefu wake mkubwa katika ukufunzi.

"Tulitulia kwa Mulee kwa sababu ni mmoja wa makocha wazoefu tulionao. Pia tuko kwenye mbio za ubingwa na ninaamini tukiwa naye tunaweza kuweka historia na klabu kwa kutwaa ubingwa msimu huu," aliambia Nation.

James Ombeng, ambaye alikuwa amechukua mikoba ya kocha Ibrahim Mohammed aliyeondoka katika klabu hiyo mwezi Februari mwaka huu, sasa atarejea tena kwenye majukumu yake kama mkufunzi wa makipa.

Kwa sasa, Gakpo imekalia nafasi ya pili kwenye jedwali la KWPL  kwa alama 31, nyuma ya Vihiga Queens ambao wana alama sawa.

Katika mahojiano ya awali, Ghost alifichua kwamba kuwa kocha wa timu ya taifa ya ilikuwa ndoto yake kuu tangu utotoni.

Mtangazaji huyo mahiri alifichua kuwa alianza kukimbiza ndoto yake ya kuwa kocha akiwa katika shule ya upili.

"Kambumbu imekuwa ndiyo ilikuwa maisha yangu. Nilitaka kuwa kocha wa timu ya taifa. Mungu alinibariki nikawa kocha wa taifa, ilikuwa ni ndoto yangu tangu nikiwa na umri wa miaka 13, nafikiri nilikuwa katika kidato cha pili," alisema kwenye mahojiano na mwandishi Samuel Maina Novemba mwaka jana.

Kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alifichua kuwa alifanikiwa kutwaa taji lake la kwanza kama kocha akiwa katika kidato cha tatu.

Ghost alieleza fahari yake kwa kuweza kuiwakilisha Kenya kama kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka kwa mara tatu.

"Matarajio yangu yalikuwa kuwa kocha hasa wa timu ya taifa, na Mungu alinifaidi, nimekuwa kocha mara tatu. Nimeitwa, nikafutwa, nikaitwa tena na nikafutwa, mpaka siku ya mwisho. Nashukuru," alisema.

Mtangazaji huyo wa kipindi cha asubuhi hata hivyo alisema kuwa mara ya mwisho alihudumu kama kocha wa taifa ilikuwa ndio mwisho wake na akaweka wazi kuwa hatazamii kuchukua nafasi hiyo tena.

Wakati huo, alifichua kuwa  anajihusisha na shughuli zingine zinazohusiana na kandanda ikiwa ni pamoja na kusimamia shule yake ya Liberty Sports Academy ambayo ilimtoa mshambulizi Michael Olunga.

"Mimi pia ni mwalimu wa wakufunzi hapa nchini. Pia mimi ni mwanachama wa Makocha hapa nchini, tuna mfumo unaojulikana kama KEFOCA. Kwa umbali, pia natangaza mambo ya kambumbu," alisema.