Wanyama atoa masharti kabla ya kurejea Harambee Stars

Mchezaji huyo ametaka masuala kadhaa kushughulikiwa kabla ya kufanya uamuzi wa kurejea.

Muhtasari

•Nahodha huyo wa zamani wa Harambee Stars amesema aamekuwa akishinikizwa kurejea katika kikosi cha taifa.

•Wanyama alisema kwamba tayari amemweleza waziri Namwamba na kocha Firat kuhusu anayotaka yashughulikiwe

Mchezaji wa Harambee Stars Victor Wanyama na Waziri Ababu Namwamba
Image: TWITTER// ABABU NAMWAMBA

Aliyekuwa nahodha wa Harambee Stars, Victor Mugubi Wanyama ameweka wazi kuwa anahitaji muda zaidi wa kufikiria kabla ya kufanya maamuzi kuhusu iwapo atarejea kwenye timu hiyo ya taifa ya soka nchini.

Akizungumza na BBC Sports Africa, Mchezaji huyo wa klabu ya Montréal Impact nchini Canada alifichua kuwa waziri wa michezo na sanaa, Ababu Namwamba na kocha wa Harambee Stars  Engin Firat wamekuwa wakimshinikiza kurejea katika kikosi cha taifa baada ya kustaafu mwaka wa 2021.

Wanyama hata hivyo ametaka masuala kadhaa kushughulikiwa kabla ya kufanya uamuzi, likiwemo suala la kocha wa kudumu.

"Ni ngumu kidogo kwa sababu tuna wachezaji wengi wazuri lakini tatizo limekuwa hawakutulia kwa kocha mmoja... Kuwa na makocha tofauti wakibadilisha wachezaji wakati wote ni ngumu," Wanyama alisema.

Kiungo huyo wa kati alieleza imani yake kwamba wasimamizi wa soka nchini wameamua kumpa Firat nafasi ya kutengeneza timu ya taifa.

Alisema kwamba tayari amemweleza waziri Namwamba na kocha Firat kuhusu anayotaka yashughulikiwe kwanza huku akidokeza kuwa huenda akarejea kwenye timu ya taifa baada ya suluhu kupatikana.

"Nilizungumza na waziri na nikazungumza na kocha (mpya). Wote wananiomba nirudi lakini nikasema 'Ninahitaji muda kidogo kufikiria kuhusu hili'.

"Labda naweza kurudi kusaidia timu, kusaidia wachezaji chipukizi wanaokuja waweze kuelewa maana ya kuwakilisha nchi yao...Nadhani wachezaji wanastahili kushughulikiwa vizuri  na taaluma zaidi," alisema.

Mwezi Desemba mwaka jana, Wanyama alishiriki kikao na waziri Namwamba kuhusu kurejea kwake katika Harambee Stars.

Katika taarifa yake baada ya mkutano huo, Namwamba alidokeza kuwa mchezaji huyo wa zamani wa Tottenham Hotspurs angerejea kikamilifu kwenye kikosi cha taifa cha soka kufuatia mazungumzo yao.

"Nimefurahia kuwa Victor Wanyama amekubali kurejea kikamilifu Harambee Stars, na kubatilisha uamuzi wake wa awali wa kujiondoa kwenye timu hiyo," Namwamba alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Wanyama alitangaza kujiondoa kwenye timu ya Taifa Harambee Stars mwezi Septemba 2021. Alikuwa nahodha tangu 2013 alipochukua nafasi ya Dennis Oliech.