Mshambulizi wa klabu ya Arsenal Bukayo Saka ameomba msamaha kufuatia uchezaji wake duni wakati wa mechi dhidi ya Westham siku ya Jumapili.
Wanabunduki walipoteza pointi mbili siku ya Jumapili mchana baada ya kutoka sare ya 2-2 na The Hammers kwenye Uwanja wa London Stadium.
Katika taarifa yake baada ya mechi hiyo, mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 21 alisema kuwa anakubali uwajibikaji wake katika matokeo hayo ya kuvunja moyo kwa mamilioni ya mashabiki wa Arsenal.
"Licha ya matokeo, Nitakubali wajibu wangu daima," Saka alisema kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.
Huku akiomba msamaha kwa wanabunduki, mshambulizi huyo aliahidi kufanya kadri ya uwezo wake kurekebisha hali.
"Naomba msamaha wanabunduki, nitafanya kila niwezalo kuifanya iwe sawa," alisema.
Wanabunduki walikuwa na matumaini ya kuendeleza uongozi wao mkubwa kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza siku ya Jumapili lakini Westham ikaangamiza ndoto yao kupitia mabao ya Said Benhrahma na Jarod Bowen.
Gabriel Jesus na Martin Odegaard walikuwa wametangulia kufunga katika dakika ya saba na ya kumi mtawalia na kuwaweka wanabunduki kifua mbele kabla ya Saka kushindwa kufunga penalti katika dakika ya 52.
Mkwaju wa penalti wa Saka ulienda nje ya lango baada ya mwamuzi wa kati kuiadhibu Westham kufuatia kosa la Michail Antonio kushika mpira wa mkono. Baadhi ya mashabiki wa Arsenal wamemlaumu mshambuliaji huyo wa Uingereza kwa sare hiyo wakisema alipaswa kufunga penalti hiyo.