Dalot asherehekea mara 5 kwa mpigo baada ya kufunga bao la kwanza tangu 2018

Beki huyo alicheza mechi yake ya kwanza ndani ya jezi ya United mwaka 2018 lakini hajawahi funga bao hata moja hadi pale alipovunja laana hiyo Jumapili.

Muhtasari

• United waliibuka washindi kwa mabao mawili kapa.

• Katika mahojiano tata na Piers Morgan, Ronaldo aliwahi sema kuwa Dalot ndiye kinda pekee aliyekuwa akimuonesha heshima United.

Diogo Dalot akisherehekea kwa mbinu tofauti tofauti.
Diogo Dalot akisherehekea kwa mbinu tofauti tofauti.
Image: Twitter//Manchester News

Beki wa Manchester United Diogo Dalot aligeuka gumzo la mitandaoni baada ya kutoa maonyesho matano tofauti akisherehekea bao lake la kwanza kama mchezaji wa Red Devils.

Mchezaji huyo ambaye anacheza nafasi ya majeruhi Luke Shaw alikuwa kwenye ubao wa wafungaji katika mechi ya Nottingham Forest dhidi ya Manchester United usiku wa Jumapili.

Kulingana na Sports Brief, mchezaji huyo ambaye alifunga bao la pili baada ya mfungaji wa bao la kwanza Antony kumpakulia bonge la asisti alifurahi ajabu na kukimbia uwanjani akisherehekea kwa mbinu tano tofuati.

“Lilikuwa bao ambalo ni wazi lilikuwa na maana kubwa kwa nyota huyo wa Ureno, ambaye alikimbilia kwenye bendera ya kona kwa msisimko na kufanya sherehe tano tofauti,” Sports Brief walidadisi.

Alianza kwa kuangalia kwa kejeli mapigo yake ya moyo, kabla ya kukimbilia kwa mashabiki wa Manchester United. Kupeana mikono na Anthony kulifuata na wawili hao wakapiga picha kwa sekunde chache katika sherehe tofauti kabisa.

Aliporudi kwenye nafasi yake, alicheza ishara ya ‘C’ na mashabiki walishangaa sana beki huyo wa kushoto akionyesha kile ambacho muda huo ulimaanisha kwake.

Tangu kushiriki mechi yake ya kwanza kwa United mwaka 2018, kulimchukua takribani miaka 5 kupata bao lake la kwanza na wakati huo ulidhihirisha furaha yake akitoa maonyesho yote ya kusherehekea ambayo amekuwa akiweka akibani.

Ikumbkwe katika mahojiano tata Novemba mwaka jana, Christiano Ronaldo alimwambia mwanahabari Piers Morgan kwamba Dalot ndiye kinda pekee aliyekuwa akimsikiliza katika timu ya United, akisema kuwa dogo huyo atakuwa na mustakabali angavu sana katika taaluma ya soka.