Mwanasoka chipukizi wa Kenya kujiunga na Real Madrid

Ndegwa Kung'u amealikwa kufanya majaribio ya vipaji katika Real Madrid.

Muhtasari

•Ndegwa Kung'u amepata mwaliko maalum wa kuhudhuria majaribio ya vipaji ya klabu hiyo ya Uhispania mwezi Juni.

•Hivi majuzi, Aymen Onyango, alifanikiwa kujiunga na timu ya Manchester City ya wachezaji wa chini ya umri wa miaka 9.

amealikwa kujiunga na Real Madrid
Ndegwa Kung'u amealikwa kujiunga na Real Madrid
Image: HISANI

Siku chache tu baada ya mwanasoka chipukizi wa Kenya, Aymen Onyango, kujiunga na akademi ya soka ya Manchester City, mchezaji mwingine mdogo kutoka Kenya anakaribia kujiunga na akademi ya Real Madrid.

Ndegwa Kung'u, 10, mwenye makazi yake Kanada amepata mwaliko maalum wa kuhudhuria majaribio ya vipaji ya klabu hiyo ya Uhispania mwezi Juni, ambapo iwapo atafaulu, ataweza kujiunga na akademi yao.

Picha ya mwanasoka huyo chipukizi mwenye kipaji kikubwa akiwa amesimama na wakufunzi wawili wa akademi ya Real Madrid huku akiwa ameshikilia cheti imeshirikishwa kwenye mitandao ya kijamii.

Hivi majuzi, mtoto wa meneja wa maendeleo katika Ligi ya Raga ya Kenya, Lucas Onyango, Aymen Onyango, alifanikiwa kujiunga na timu ya Manchester City ya wachezaji wa chini ya umri wa miaka tisa.

Bw Onyango alizamia kwenye mtandao wa Twitter takriban wiki moja iliyopita kufichua habari hizo:

Mtoto wetu Aymen Onyango sasa ni mchezaji rasmi wa Manchester City baada ya kusajiliwa kwa vijana wa chini ya miaka 9. Katika maisha yangu sijawahi kujivunia hivi na kijana huyu amefanya bidii kufika hapa, safari inaanza sasa hivi anaendelea na akademi. . Sote tumefurahi," Onyango alitweet.

Baadhi ya wachezaji wengine chipukizi wa Kenya wamefanikiwa kujiunga na akademi za vilabu vikubwa vya Ulaya katika miaka ya hivi majuzi.

Mwaka wa 2021, mwanasoka mchanga wa Kenya, Leo Messo alijunga na akademi ya Arsenal akiwa na umri wa miaka 10.

Wengine ni pamoja na:-

  • George Gitau alijiunga na Middlesbrough 2020 na miaka 16.
  • Brooklyn Kazungu alijiunga na Leicester 2017 na miaka 9
  • Zech Obiero alijiunga na Tottenham 2015 na miaka 8
  • Tyler Onyango alijiunga na Everton 2011 na miaka 8
  • Clarke Odour alijiunga na Leeds 2010 na miaka 10
  • Silko Thomas alijiunga na Chelsea tarehe isiyothibitishwa.