Klopp apata jeraha na misuli ya paja akisherehekea bao la ushindi dakika za mwisho

Mechi hiyo ilionekana kumalizika kwa sare ya 3-3 lakini bao la Diogo Jota kunako dakika ya 94 kuliipatia Liverpool alama zote tatu .

Muhtasari

• Liverpool walitangulia kufunga mabao 3 chini ya dakika 15 za kwanza na kabla ya kipindi cha mapumziko, wageni walirejesha bao  moja kupitia Harry Kane.

• Kipindi cha pili Spurs walirejesha mabao mengine mawili na kufanya mechi kuwa sare 3-3 hadi dakika za mwisho kabisa kabla ya Jota kuipa Liverpool ushindi.

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp alishikilia misuli yake baada ya kupata jeraha.
Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp alishikilia misuli yake baada ya kupata jeraha.
Image: Twitter

Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp alionekana kupata jeraha la misuli yake ya paja katika mazingira ya kutatanisha baada ya Diogo Jota kufunga bao la dakika za mwisho katika ushindi wa 4-3 dhidi ya Tottenham Jumapili.

The Reds walikimbia kwa mabao 3-0 dhidi ya wageni wao walioshindwa kwenye Uwanja wa Anfield huku Curtis Jones na Luis Diaz wakifunga ndani ya dakika 5 za kwanza. Mohamed Salah aliongeza la tatu kwa mkwaju wa penalti dakika ya 15 na kuwaacha Spurs na mlima wa kupanda.

Lakini washika mitutu hao wa London, wakiongozwa na kocha mkuu wa muda Ryan Mason, walipata bao moja la kuvuta machozi kabla ya kipindi cha mapumziko kupitia kwa Harry Kane. Na mabao ya kipindi cha pili kutoka kwa Son Heung-min na Richarlison yalionekana kufikisha pointi isiyotarajiwa kwa Spurs kabla ya Jota kuibuka dakika ya 94 na kuzamisha jahazi la Spurs dakika za zima taa tulale.

Kutokana na ushindi huo usiotarajiwa wa Liverpool dakika za mwisho, kocha wao Jurgen Klopp aliruka kwa mbwembwe baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa pindi tu baada ya Jota kufunga bao la ushindi.

Kuruka kwake kwa furaha hata hivyo kulimzalishia jeraha la misuli ya oaja ambapo alionekana akijishika upande wa nyuma wa paja lake la mguu wa kulia.

Klopp alipewa kadi ya njano mara moja na mwamuzi Paul Tierney kwa ubwatukaji wake wa hali ya juu. Lakini Gary Neville, ambaye alikuwa akitoa maoni yake kuhusu mechi katika runinga ya Sky Sports, alidai kuwa Mjerumani huyo alipaswa kuona kadi nyekundu kwa tabia yake kwenye pembe za chaki.