Napoli wameshinda taji lao la kwanza la Serie A kwa miaka 33 walipotoka sare na Udinese kwenye uwanja wa Dacia Arena na kuibua shangwe kubwa huko Naples.
Walishinda ligi mara ya mwisho mwaka wa 1990 huku timu iliyoongozwa na Diego Maradona ikiongeza taji lao la kwanza miaka mitatu nyuma.
Victor Osimhen alifunga bao la kusawazisha dakika ya 52 baada ya Sandi Lovric kuipatia Udinese bao la kuongoza. Na Napoli walishikilia hatua waliyohitaji kushinda taji lao la tatu la Serie A zikiwa zimesalia mechi tano.
"Kuona wana Napoli wakiwa na furaha inatosha kukupa hisia ya furaha wanayohisi," bosi wa Napoli Luciano Spalletti aliiambia DAZN.
"Watu hawa wataangalia wakati huu ambapo maisha yatakuwa magumu, wana haki ya kusherehekea hivi. Unajisikia utulivu zaidi ukijua kuwa umewapa wakati huu wa furaha."
Napoli inamaliza miongo mitatu ya maumivu. Mataji mawili ya awali ya Napoli yalikuja katika siku za nguli wa Argentina Maradona - ambaye uwanja wao sasa unaitwa - mnamo 1987 na 1990.
Kufuatia siku hizo za utukufu klabu ilianguka katika mdororo wa kifedha, kushuka daraja na kufilisika; ikicheza Serie C hivi majuzi mwaka 2006.