Messi aomba radhi kwa kusafari Saudi Arabia bila idhini

"Kwa kweli nilifikiri tungekuwa na siku ya mapumziko baada ya mechi kama ilivyokuwa wiki zilizopita.

Muhtasari
  • Messi anakaribia kuondoka PSG mkataba wake utakapomalizika majira ya joto.
Image: HISANI

Lionel Messi amewaomba radhi wachezaji wenzake wa klabu ya Paris St-Germain na kusema kuwa atasubiri klabu hiyo kuamua hatua itakayochukua dhidi yake baada ya kufanya safari bila kibali nchini Saudi Arabia.

Nahodha huyo wa Argentina alisimamishwa na klabu hiyo kwa wiki mbili kwa ajili ya safari hiyo.

Ilifuatia PSG kushindwa nyumbani na Lorient siku ya Jumapili - la tatu katika mechi sita - wakati Messi alicheza dakika 90.

"Naomba radhi kwa nilichofanya na nasubiri kuona klabu itaamua nini," Messi alisema kwenye video iliyowekwa kwenye mtandao wa Instagram.

"Kwa kweli nilifikiri tungekuwa na siku ya mapumziko baada ya mechi kama ilivyokuwa wiki zilizopita.

"Nilikuwa nimepanga safari hii kwenda Saudi Arabia baada ya kuighairi hapo awali. Wakati huu sikuweza kuighairi."

Messi anakaribia kuondoka PSG mkataba wake utakapomalizika majira ya joto.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35, ambaye pia amepigwa faini na klabu hiyo, ana jukumu la kuwa balozi wa utalii wa Saudi Arabia.

Meneja wa PSG Christophe Galtier anasema "hakuwa na uhusiano wowote na" kusimamishwa kwa Messi, huku pia akilaani maandamano ya mashabiki nje ya nyumba za wachezaji.