Kinda mwenye talanta ya soka aitema Kenya, achagua kuchezea Ubelgiji

Kinda huyo wa miaka 21 alizaliwa kwa mama Mkenya na baba Mkongo na kulelewa Ubelgiji.

Muhtasari

• Kulikuwa na matumaini kutoka Kenya hasa kwamba kijana huyo mwenye umri wa miaka 21 angechagua kuwakilisha nchi aliyozaliwa mama yake katika ngazi ya juu.

Eliot Matazo, beki wa AS Monaco.
Eliot Matazo, beki wa AS Monaco.
Image: Getty Images

Mshambulizi wa Harambee Stars Eliot Matazo anaonekana kumaliza uvumi kuhusu soka lake la kimataifa kwa kukiri kwamba anatazamia kuiwakilisha timu ya taifa ya wakubwa ya Ubelgiji.

Kinda huyo wa AS Monaco alizaliwa nchini Ubelgiji kwa baba Mkongo na mama Mkenya. Tayari amechezea timu za Ubelgiji za chini ya miaka 16, 18 na chini ya miaka 21 na sasa anabisha hodi kwenye mlango wa timu ya wakubwa, jambo ambalo anatamani sana kufanikiwa.

Kulikuwa na matumaini kutoka Kenya hasa kwamba kijana huyo mwenye umri wa miaka 21 angechagua kuwakilisha nchi aliyozaliwa mama yake katika ngazi ya juu, lakini mchezaji huyo anaonekana kuwa na mipango mingine na analenga kuichezea nchi yake ya kuzaliwa pekee.

Katika mahojiano, kiungo huyo wa kati wa safu ya ulinzi alisema amekuwa akifurahia kujitokeza katika timu ya vijana chini ya umri wa miaka 21 na akabainisha kuwa kuna wachezaji wengi wenye vipaji katika kundi hilo.

"Ninajisikia vizuri katika mazingira hayo. Kila wakati ninapoenda uwanjani na Vijana wa U21, ninachukua jukumu zaidi, na ninahisi hivyo kutoka kwa kocha pia. Tuna kizazi kizuri, kikundi kizuri kinachofanya vyema, na ninapenda kwenda huko. Najisikia vizuri huko, na nina furaha kuwa huko," aliiambia getfootballnewsfrance.com.

Anaongeza kuwa anatarajia kujitokeza kwenye timu ya wakubwa na pia alifichua kuwa anafahamu kuwa kocha mpya wa timu ya taifa, Domenico Tedesco, amekuwa akimfuatilia kwa karibu.

“Nafikiri haya mambo yanatokea kwa kawaida, ukifanya vizuri na klabu yako na ukifanya vizuri utapigiwa simu, muda ukifika nitakuwa tayari kwa sababu najua nitakuwa nimeshafanya kazi. kufika huko, pamoja na Vijana wa U21 na pia Monaco. kuhakikisha ninajitolea vilivyo bora ili aweze kunitazama zaidi," aliongeza.