Mikel Arteta awaomba radhi mashabiki wa Arsenal huku matumaini ya ubingwa yakififia

Meneja huyo alikiri kwamba timu yake haikujitolea katika kipindi cha pili cha mechi ya Jumapili.

Muhtasari

•Arsenal walipata pigo kubwa baada ya Brighton & Hove Albion kufanya matumaini yao ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza kufifia.

•Baada ya kipigo hicho cha kuvunja moyo, kocha Mikel Arteta aliomba radhi kwa mamilioni ya mashabiki wa Arsenal kwa kuwaangusha.

•Arteta hata hivyo alibainisha kuwa timu yake changa imefanya vyema msimu huu na hata kuvuka matarajio ya wengi.

Mikel Arteta wa Arsenal
Mikel Arteta wa Arsenal
Image: GETTY IMAGES

Siku ya Jumapili, Arsenal walipata pigo kubwa baada ya Brighton & Hove Albion kufanya matumaini yao ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza kufifia.

Wanabunduki walipokea kichapo cha aibu cha 0-3 nyumbani kwa mabao ya Julio Enciso, Deniz Undav na Pervis Estupinian mara tu baada ya washindani wao wakuu msimu huu, Man City kuboresha nafasi zao za ubingwa kwa kuwafunga Everton 3-0.

Baada ya kipigo hicho cha kuvunja moyo, kocha Mikel Arteta aliomba radhi kwa mamilioni ya mashabiki wa Arsenal kwa kuwaangusha.

"Ni hisia tofauti kabisa na hisia ambayo sote tulikuwa nayo siku ya Jumapili iliyopita [dhidi ya Newcastle] tulipojivunia na tulihisi kwamba tulifanya kile tulichohitaji kushinda katika nyakati fulani. Leo (Jumapili) ni kinyume kabisa. Inabidi tuwaombe radhi watu wetu hasa kwa kipindi cha pili," Arteta aliwaambia wanahabari baada ya mechi.

Meneja huyo mwenye umri wa miaka 41 alikiri kwamba timu yake haikujitolea katika kipindi cha pili cha mechi ya Jumapili.

Alisema mchezo hafifu katika kipindi hicho  haukubaliki na kudokeza kuwa hatua zitachukuliwa kuzuia hilo siku zijazo.

"Tulipambana sana kuwa katika nafasi tuliyo nayo na leo tulikuwa katika wakati mgumu wa kuweka matumaini na kufanyia kazi ndoto hiyo. Unapolazimika kucheza katika dakika hizi huwezi kufanya kile tulichofanya kipindi cha pili. Ikiwa timu ina uwezo wa kufanya hivyo inapofikia hatua kubwa zaidi, kuna mambo mengi ya kuchambua na kufikiria kwa sababu hayawezi kutokea," alisema.

Arteta hata hivyo alibainisha kuwa timu yake changa imefanya vyema msimu huu na hata kuvuka matarajio ya wengi.

Kuhusu kutoendeleza matokeo mazuri hadi mwisho wa msimu, kocha huyo wa Uhispania alisema anaomba radhi kwa hilo.

"Ni wazi kile ambacho timu imefanya katika kipindi cha miezi 10 iliyopita ni tofauti sana na kile ambacho mtu yeyote alitarajia na hilo huleta matarajio mengi pamoja na shauku, furaha na shangwe. Hilo ni jambo ambalo linapaswa kusimamiwa kwa njia sahihi na baada ya hapo tuna jukumu la kuhakikisha timu inafanya kazi na ninawajibika kwa hilo. Kwa hivyo nachukia hisia za kuwakatisha tamaa watu wanapotarajia jambo fulani. Hayo ndiyo majuto makubwa niliyonayo leo na sina budi kuomba msamaha kwa hilo.” Alisema.

Kwa sasa, wanabunduki wamekalia nafasi ya pili kwa pointi 81 huku wakiwa wamebaikisha mechi mbili pekee. Viongozi Man City kwa upande wao wako na alama 85 huku bado wakiwa na mechi tatu za kucheza.