Aubameyang ashinda taji la Laliga na Barcelona licha ya kuhamia Chelsea

Mshambulizi huyo amejumuishwa kwenye kikosi cha Barca kilichoshinda taji licha ya kuchezea klabu hiyo dakika 8 tu msimu huu.

Muhtasari

•Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 33 amejumuishwa kwenye kikosi cha  Barcelona kilichoshinda taji la Laliga 2022/23.

•Alicheza dakika nane pekee katika mchuano wa kwanza wa msimu wa klabu hiyo ya Uhispania dhidi ya  Rayo Vallecano.

Mshambulizi wa Chelsea Pierre Emerick Aubameyang
Image: HISANI

Mwanasoka wa Gabon Pierre Emerick Aubameyang ameshinda taji lake la kwanza la ligi baada ya kuchezea vilabu na ligi mbalimbali akitafuta ushindi.

Licha ya kuhamia Chelsea mapema mwaka huu na kushiriki katika mechi kadhaa za klabu hiyo ya Uingereza, mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 33 amejumuishwa kwenye kikosi cha  Barcelona kilichoshinda taji la Laliga 2022/23.

Barcelona walinyakua taji la Uhispania Jumapili baada ya kuwapiga Espanyol 4-2. Walishinda kwa pointi 85 bado wakiwa na mechi 4 mkononi.

Licha ya kuwa na kipindi kibaya katika Chelsea ndani ya takribani miezi 5 iliyopita, mshambuliaji huyo ana la kusherehekea baada ya kujumuishwa kwenye kikosi kilichoshinda Laliga 2022/23 cha Barcelona licha ya kuwa ameichezea klabu hiyo mechi moja pekee msimu huu. Alicheza dakika nane pekee katika mchuano wa kwanza wa msimu wa klabu hiyo ya Uhispania dhidi ya  Rayo Vallecano.

Huku hayo yakijiri, ni wazi kuwa nahodha huyo wa zamani wa Arsenal hana mpango wa kusalia Stamford Bridge baada ya msimu wa 2022/23 kukamilika.

Hivi majuzi, nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 alidokeza nia ya kusitisha mkataba wake na Chelsea huku akishiria nia ya kurejea katika klabu hiyo ya Barcelona. Aubameyang alitia saini mkataba wa miaka miwili na The Blues baada ya kujiunga nao mnamo mwezi Septemba mwaka jana kwa uhamisho wa £10m kutoka Barcelona.

Kufuatia msimu mbaya katika klabu hiyo yenye maskani yake jijini London, nahodha huyo wa zamani wa Arsenal sasa anatazamia kuondoka Stamford Bridge mwishoni mwa msimu huu na kujaribu kufufua mchezo wake kwingineko, huku Chelsea  pia wakiashiria furaha ya kukatiza uhusiano naye.

"Ningependa kurejea Barcelona lakini tutaona," alisema Aubameyang katika mahojiano na Djam Life.

Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 33 amekuwa na kipindi kigumu katika Chelsea, akiwa amefunga mabao matatu pekee katika mechi 21. Ameachwa nje ya kikosi cha washindi wa Ligi ya Mabingwa mwaka wa 2021 mara kadhaa.

Alipoulizwa kuhusu klabu gani angependa kujiunga nayo baadaye, alisema “Sijui. Tutaona. Naipenda Barca.