Makosa 7 ambayo Arsenal walifanya na kufifisha matumaini yao ya kuibuka mabingwa EPL

Neville alisema kuwa Arsenal haifai kusingizia majeraha au shinikizo kutoka kwa Manchester City kwani walipenda wenyewe kupoteza uongozi wa pointi 8.

Muhtasari

• Mchambuzi huyo alisema kuwa kutostahimili presha kuliwaponza sana Arsenal

• Alifichua kwamba Arsenal walianza kuvurunda pale walipodondosha pointi 12 katika mechi 7 kwa njia ya kimasihara.

Arsenal wakiwa hawamini macho yao kile kinachoendelea uwanjani baada ya kichapo.
Arsenal wakiwa hawamini macho yao kile kinachoendelea uwanjani baada ya kichapo.
Image: Twitter

Beki wa zamani wa Manchester United ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa kandanda nchini Uingereza Gary Neville ameorodhesha sababu kadhaa ambazo huenda zilichangia katika matumaini ya Arsenal kuibuka mabingwa msimu huu kuona kiza kinene ghafla.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Neville alisema kuwa wachezaji na mashabiki wa Arsenal kusema ni majeraha au kuwekewa presha na Manchester City si sababu tosha kwani shinikizo kama hilo hutarajiwa aghalabu katika ligi yenye ushindani kama ya premia.

“Arsenal imekuwa na msimu mzuri sana lakini ulipozidi kuwa mgumu walitatizika. Inaonekana sasa simulizi ni kwamba ni nguvu ya City, majeraha na kukimbia kwa bidii ndio sababu. Haya ni mambo ya kawaida ambayo yanahitaji bei katika mbio za ubingwa,” Neville alisema.

Alifichua kwamba Arsenal walianza kuvurunda pale walipodondosha pointi 12 katika mechi 7 kwa njia ya kimasihara.

Neville ambaye ni mkereketwa wa Manchester United alisema kuwa Arsenal kuwa na kikosi chenye wachezaji wachanga ambao hawangeweza kustahimili shinikizo ni moja kati ya janga kuu lililoiathiri sana timu hiyo ambayo ilikuwa kifua mbele kwa alama 8 kileleni mwa jedwali.

“Kupoteza fomu, kuachana na kuongoza, nguvu na miguu kwenda, kufanya makosa yasiyotarajiwa ambayo hayakuonekana mwanzoni mwa msimu, wachezaji wachanga wanakuwa na wasiwasi na kupoteza uhuru wao wa kujieleza na wengine kuonyesha hisia nyingi wakati utulivu unahitajika,” Neville alisema.

Mchambuzi huyo alisema kuwa kutostahimili presha kuliwaponza sana Arsenal na kusisitiza umuhimu wa timu kuwa na wachezaji wenye tajriba na kuhimili nyakati ngumu na uzoefu mkubwa.

“Hata hivyo katika mazingira ya utendaji wa juu na katika ngazi ya upekee lazima bado tutambue wakati shinikizo limechukua mkondo wake. Natumai wachezaji hawa wa Arsenal watachipuka tena siku moja (kama si United) na wanaweza kuliona hilo,” Neville alisema.