"Inauma sana, nina huzuni!" Mikel Arteta avunja kimya baada ya kuachia Man City ubingwa wa EPL

“Kwanza niwapongeze City kwa kutwaa ubingwa, lakini ni wazi kuwa ni siku ya huzuni sana kwetu!" alisema.

Muhtasari

•Arteta alikubali lawama kwa Arsenal kupoteza kasi katika awamu ya mwisho ya EPL 2022/23 huku akiipongeza Man City kwa kushinda kombe hilo la Uingereza.

•Alisema mabao mengi ambao timu yake imeruhusu washindani wao kufunga yamewagharimu sana katika mbio za ubingwa.

Mikel Arteta wa Arsenal
Mikel Arteta wa Arsenal
Image: GETTY IMAGES

Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta alikubali lawama kwa klabu hiyo kupoteza kasi katika awamu ya mwisho ya mbio za ubingwa wa  EPL 2022/23 huku akiipongeza Manchester City kwa kushinda kombe hilo la Uingereza.

Siku ya Jumamosi jioni, klabu hiyo yenye maskani yake London ilipokea kichapo cha 1-0 ugenini dhidi ya Nottingham Forest ambao walikuwa wakipigania kukwepa kushushwa daraja. Kipigo hicho kilimaanisha kwamba vijana hao wa Arteta hawana nafasi ya kuisimamisha City katika mechi chache zilizosalia.

“Kwanza niwapongeze City kwa kutwaa ubingwa, lakini ni wazi kuwa ni siku ya huzuni sana kwetu baada ya kila kitu tulichofanya msimu huu," Mikel Arteta aliambia Sky Sports baada ya mechi dhidi ya Nottingham.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 41 alikiri kwamba timu yake iliruhusu bao rahisi na ilikosa nguvu ya kutosha kuvunja Nottingham Forest  ambao kwa sasa wamekalia nafasi ya 16 wakiwa na pointi 37 pekee.

"Tungeweza kucheza hapa kwa saa tatu na nina hisia kwamba hatukuwa na nguvu ya kutosha [kufunga]," alisema.

Alisema mabao mengi ambao timu yake imeruhusu washindani wao kufunga yamewagharimu sana katika mbio za ubingwa.

"Hatupaswi kutafuta visingizio na kutafuta kuweka hatia kwa mtu. Tunapaswa kuwa bora kama timu. Tulipaswa kuwa bora kama timu na katika wiki chache zilizopita tumekosa, hiyo ni hakika," alisema meneja huyo.

Arteta alikiri sasa ni wakati wa timu hiyo pamoja na mashabiki wake kuponya maumivu ya moyo baada ya kuwa na matumani ya kutwaa ubingwa wa EPL kwa siku nyingi na mwishowe ndoto hiyo kuponyoka katika siku za mwisho.

"Tumeshindana lakini hatukutosha. Sasa lazima tupone. Inauma sana. Nina huzuni sana. Lazima nitafute njia ya kuwainua wachezaji na tuna wiki ngumu mbele yetu,"

Licha ya huzuni hiyo, meneja huyo Mhispania aliwaahidi mashabiki wa Arsenal mechi nzuri ya mwisho ya msimu huu dhidi ya Wolves wikendi ijayo kuona kwamba watakuwa wakicheza kwenye uwanja wa nyumbani.

Man City ndio washindi rasmi wa EPL 2022/23 wakiwa na mechi tatu mkononi. Wameratibiwa kumenyana na Chelsea leo mchana.