KANDANDA HUDUNDA

Laana? Kwa nini Chelsea hawajafunga City katika michuano 6 iliyopita

Tangu 2021 Chelsea hajamfunga Man City Katika mashindano yote.

Muhtasari

•Mara ya mwisho Chelsea kupata ushindi dhidi ya Man City  ilikuwa  mwaka wa 2021, katika finali ya  ligi ya mabingwa bara Ulaya.

•Chelsea imeweza kukutana na City katika safari sita  kwenye mashindano yote huku klabu hiyo ya London ikiwa imepoteza  mechi  zote hizo.

Mara ya mwisho Chelsea kupata ushindi dhidi ya Man City  ilikuwa  mwaka wa 2021, katika finali ya  ligi ya mabingwa bara Ulaya, ambapo City alipoteza 1-0 katika mchuano huo uliojawa na mbwembwe.

Bao hilo la kipekee la Chelsea lilitiwa wavuni na Mjerumani Kai Havertz katika dakika ya 42 ya mechi hiyo na kumtunuku kocha Thomas Tuchel taji hilo muhimu katika msimu wake wa kwanza akiwa Chelsea.

Tangu wakati huo,Chelsea imeweza kukutana na City katika safari sita  kwenye mashindano yote huku klabu hiyo ya London ikiwa imepoteza  mechi  zote hizo  na kufungwa jumla ya mabao 10-0.Kwa sasa katika ligi kuu Uingereza, Chelsea amekalia nafasi ya kumi na mbili kwenye jedwali kwa alama 43 baada ya mechi 36 huku ikiwa imefungwa mabao 42.

City iliwabandua The Blues  kwenye pambano la taji la FA, kwa kuwafunga mabao 4-0 kabla ya kukutana mara mbili kwenye ligi kuu  Uingereza,  ambapo vijana hao wa Pep Guardiola wamepata ushindi bila fungwa bao. Kauli inayoibuka ni kwamba, bao lake Havertz ndilo lilikuwa la mwisho kwa Chelsea kumfunga City?

Haya yanajiri huku aliyekuwa kiungo wa City Raheem Sterling akipoteza nafasi nyingi za wazi zilizochangia Chelsea kupoteza mechi dhidi ya City ugani Etihad siku ya Jumapili na kisha  kuendeleza matokeo duni chini ya ukufunzi wa Frank Lampard.

Lampard,aliteuliwa kaimu meneja kufuatia kupigwa kalamu kwa Graham Potter mwanzoni  mwa Aprili. Tangu kurejea kwake  ugani Stamford Bridge, Chelsea imepoteza mara nane na kupiga sare mbili na kisha kupata ushindi mara moja katika mashindano yote. 

Man City ambao wapo mbioni kuyasaka mataji matatu msimu huu,walivikwa taji la kwanza Jumapili 21 Mei  kwa kumpiku Arsenal huku wakiwa na uchu wa kulinyakua taji la ligi ya mabingwa.