Kocha wa Manchester United Erik Ten Hag aliweka bayana kuwa alihitaji kunusuru nafasi ya nne bora ndipo kushiriki katika shindano la ligi ya mabingwa kuliko kusubiri wikendi watakapokuwa wakichuana na Fulham katika mechi ya kuhitimisha msimu wa 2022/2023.
Vijana hao wa Ten Hag walipata uongozi muda wa dakika sita ya mchezo wakati Casemiro alipounganisha mwaju wa ikabu kutoka kwa Christian Eriksen kabla ya bao la Antony Martial kumalizia kipindi cha kwanza kwa wenyeji.
Wenyeji hao wa Old Trafford waliendelea kuidhalilisha Chelsea wakati walipofunga bao jingine kupitia mkwaju wa penati kunako dakika ya 73 kabla ya Mwingereza Rashford kumaliza mchezo dakika ya 78 kwa bao la nne.
Chelsea, licha ya kitumbua chao kuingia mchanga walipata bao la kufutia machozi kutoka kwa Joao Felix dakika ya 89 ya mchezo wakati mechi ilipotamatika kwa 4-1 kwa faida ya Man U.
Manchester United ambao tayari wamelinyakua taji la Carabao,tarehe 3 mwezi Juni watakuwa na kibarua katika fainali ya kombe la FA dhidi ya mabingwa wa ligi ya Premier City,huku kila mmoja akiwa na uchu wa kulipata taji hilo ugani Wembley.
Haya yanajiri huku mchezo wa vigogo wa soka Chelsea, kuendelea kudorora na kocha Frank Lampard kuendelea kuonesha matokeo mabaya.Baada ya bao la kwanza la United,kamera zote uwanjani Old Trafford ziliangaziwa kwake huku mikono yake ikiwa pamoja.
Tangu alipoichukua mikoba kutoka kwa Graham Potter, mengi yalitarajiwa hasa kulipobainiaka kiwango cha pesa Chelsea ilitumia katika usajili wa wachezaji wapya.Amepata kushindwa mara 8 katika mechi kumi .
Iwapo bado kuna mashabiki wanaounga mkono klabu ya Chelsea,hawapaswi kufa moyo maana miezi kumi iliyopita,Manchester United ilikuwa katika hali kama hiyo wakati kocha aliyeteuliwa kwa muda mfupi Ralf Rangnick aliposhindwa kuirejesha katika hali nzuri baada Ole Gunnar Solskjaer kupigwa kalamu.