Timu itakayoshinda ligi kuu ya Kenya haitapewa kitu chochote zaidi ya makofi tu! - Ripoti

Hiyo inamaanisha, mshindi, ambaye atatoka kwa timu tatu za ama Tusker, Gor Mahia au Nzoia Sugar watashangiliwa tu na waandalizi na mashabiki wao.

Muhtasari

• Nick Mwendwa, bosi wa FKF alikuwa na uchungu alipofichua kwamba hakutakuwa na malipo ya pesa kwa washindi wote wa FKF.

Nick Mwendwa afichua mshindi wa ligi ya FKF hatolipwa kitu chochote
Nick Mwendwa afichua mshindi wa ligi ya FKF hatolipwa kitu chochote
Image: GOAL

Huku zikiwa zimesalia mechi chache kuelekea kutamatika kwa ligi kuu ya FKF nchini Kenya, ripoti mpya imeibuka kwamba mshindi wa ligi hiyo hatokabidhiwa zawadi yoyote isipokuwa kupigiwa makofi ya hongera tu basi!

Hii ni kulingana na taarifa iliyochapishwa na jarida la The Standard mtandaoni, ikionesha jinsi ligi ya mchezo wa kandanda nchini Kenya imeathirika pakubwa kifedha lakini pia kimikakati na mipangilio.

Kulingana na jarida hilo, Hiyo inamaanisha, mshindi, ambaye atatoka kwa timu tatu za ama Tusker, Gor Mahia au Nzoia Sugar watashangiliwa tu na waandalizi na mashabiki wao.

“Ligi hiyo iliyokuwa hai barani imekuwa katika tahadhari nyekundu kwa misimu kadhaa, lakini kampeni mbili zilizopita zinaonekana kuwa mbaya Zaidi,” Jarida hilo liliripoti.

Msimu wa 2021/22, Tusker walitawazwa mabingwa, lakini walijinyakulia kitita cha Shilingi milioni 2 tu kama zawadi kutoka kwa Kamati ya Uangalizi ya FKF ambayo ilikuwa imeteuliwa na aliyekuwa waziri wa Michezo Amina Mohamed kusimamia masuala ya soka nchini baada ya kuvunjwa kwa shirikisho la FKF kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha, The Standard walisema.

Baada ya kurejeshwa kwa shirikisho linaloongozwa na Nick Mwendwa, bosi wa FKF alikuwa na uchungu alipofichua kwamba hakutakuwa na malipo ya pesa kwa washindi wote wa FKF na mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya Vihiga Queens hivi majuzi kutokana na shida ya kifedha.

Lakini alikuwa mwepesi wa kuahidi msimu mkubwa na wenye faida kubwa wa 2023/24 ambao utaanza Agosti 2023 na kumalizika Mei 2024.

"Hakuna pesa na hatutawazawadia mabingwa wa ligi msimu huu. Hatutakuwa na zawadi yoyote, pesa zitatoka wapi? Huu ulikuwa msimu wa uokoaji tu. Tunaweza kutaka kujaribu na hata kuwa na shangwe, lakini hatuna takwimu na kamati ambayo ingefaa kufuatilia uchezaji wa wachezaji,” Mwendwa aliambia Standard Sports.

Taarifa hizi za kuchefua roho kwa wapenzi wa michezo nchini zinakuja siku tatu tu baada ya timu ya kitaifa ya Raga ya wachezaji saba kila upande, Shujaa kushushwa ngazi katika msururu wa raga wa dunia baada ya miaka 20.

Kwa kweli matukio ambayo yanaendelea katika tasnia ya michezo nchini yanaonesha uovu na uvundo uliokithiri na wengi wanahisi waziri wa michezo Ababu Namwamba ana kibarua kigumu kufufua michezo humu nchini na kuibua talanta kupitia mradi wa Talanta Hela.