Wikendi iliyopita kulikwa na mashindano ya Formula 1 nchini Uhispania ambapo mastaa mbalimbali walijitokeza kushabikia mchezo huo unaoenziwa katika mataifa mengi ya bara Uropa, kando na soka.
Miongoni mwa waliojitokeza kushabikia mchezo huo ni wachezaji wa Chelsea Mason Mount na Ben Chilwell na kama ilivyo kawaida ya wanahabari, hawakumpa nafasi Mount kufurahia F1 na badala yake walimkaba kwa maswali kuhusu uvumi na tetesi za kuondoka kwake Chelsea kwenda Mancheter United.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mchezaji huyo kukabwa na swali la kuondoka kwake katika klabu ya utotoni na mbaya Zaidi kuenda katika klabu ambayo ni mahasimu wa jadi wa Chelsea – Manchester United.
Katika video ambayo imekuwa ikienezwa mitandaoni, mwanahabari alionekana kumkaribia Mount na bila kupepesa jicho alimtupia swali hilo la kuondoka kwake Chelsea.
Mouth kwa upande wake alishindwa kuzuia kicheko lakini alijibu kwa kukwepa huku akisema kuwa alikuwa nchini Uhispania kwa minajili ya kujivinjari tu katika mashindano ya F1 huku akionekana kabisa kukwepa kuzungumzia uvumi huo wa kuondoka Chelsea.
"Niko hapa kufurahia tu mbio hizi leo, siku ya ajabu. Siwezi kusubiri kuitazama hapa,” Mount alisema akiweka wazi kwamba hangetaka kuzungumzia uvumi wa kuondoka kwake Chelsea kwenda United.
Mount amekuwa akihusishwa kuondoka katika klabu hiyo ya London baada ya mazungumzo kuhusu mkataba mpya kugonga mwamba kwa mara kadhaa sasa.
Kinda huyo wa Uingereza amebakisha mkataba wa mwaka mmoja katika timu hiyo na sasa Chelsea wanaripotiwa kutaka kumuuza majira haya ya joto kwa kima cha pauni milioni 70 ili kukwepa kumpoteza bila senti mwishoni mwa msimu ujao.