Mwanaume mmoja wa Ghana ambaye ni mwanasoka wa zamani anayeishi Uingereza kwa mara nyingine tena amejitokeza akisema kuwa yeye ndiye baba halisi wa mshambuliaji wa Manchester United, Muingereza Marcus Rashford.
Inaarifiwa kwamba hii si mara ya kwanza kwa mfanyibiashara huyo kuibua madai ya kuwa Rashford ni mwanawe wa kumzaa.
Michale Boye-Marquaye katika video ambayo ilipakiwa TikTok, ambaye alikuwa mwanasoka wa kulipwa zamani anashikilia msimamo wake kuwa ndiye baba wa mchezaji huyo lakini kwa muda mrefu ameamua kulinyamazia suala hiyo kwa kile alichokiita kuwa ni ‘heshima kubwa kwa mwanangu huyo’.
Marquaye sasa anasema kuwa mchezaji huyo amemghasi kwa kile alisema kuwa ni kutokuwa na haraka au uchu wa kumtafuta baba yake kwa miaka mingi sasa licha ya kuwa na mafanikio makubwa kwenye soka.
Katika video hiyo mpya, Marquaye alisema kuwa hamfuatilii mwanawe Rashford kutokana na mafanikio yake bali anachokitaka ni mwanawe kumtambua kama baba yake, basi!
“Mimi ni babako, hili suala limekuwa likiendelea kwa muda mrefu lakini niliamua kukaa kimya. Mnaweza sema chochote mtakacho. Ninamheshimu sana Melanin – mamake Rashford – pamoja na mumewe, lakini hilo halitonizuia dhidi ya kuzungumza ukweli. Kama sitakwambia ukweli, wewe, watoto wako na wajukuu wako watapotea,” Marquaye alisema.
“Sifanyi hivi kwa sababu ya pesa, ni wewe tu ambaye nataka.ninapoteza utulivu wangu, ninakuwa na hasira. Nimekaa kimya muda mrefu kwa sababu ya heshima tu. Mimi ni babako na unaweza kuja muda wowote unataka, mikono yangu i wazi kukukaribisha.”
Matamshi ya Marquaye yanakuja siku chache baada ya mamake Rashford kufunguka kwenye mahojiano kuhusu jinsi alipitia wakati mgumu akiwalea watoto wake.
“Nilikuwa nawaambia wanangu kwamba tayari nimeshakula kwa sababu wangeniuliza mbona sili nao. Lakini ukweli ni kwamba sikuwa nimekula na nilikuwa nataka kuwaona wanangu wako vizuri tu. Sasa Marcus amenipatia nyumba na wakati mwingine naketi kwenye chumba change na kulia tu. Kufikiria kwenye nimetoka na kwenye nimefikia sasa,” mamake Rashford alizungumza kwenye mahojiano hayo.