Wanabunduki watangaza usajili wa Kai Havertz huku Declan Rice akikaribia kujiunga na klabu hiyo

Ni rasmi kuwa mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani Kai Havertz mchezaji wa Arsenal.

Muhtasari

•"Kiungo wa kimataifa wa Ujerumani Kai Havertz amejiunga nasi kutoka Chelsea kwa mkataba wa muda mrefu," Arsenal ilitangaza.

• Wanabunduki wanaripotiwa kumsajili fowadi huyo mwenye umri wa miaka 24 kwa pauni milioni 65.

amejiunga na wanabunduki
Kai Havertz amejiunga na wanabunduki
Image: TWITTER// ARSENAL

Ni rasmi kuwa mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani Kai Havertz mchezaji wa Arsenal.

Wanabunduki walitangaza usajili wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 kutoka Chelsea kupitia tovuti yake rasmi siku ya Jumanne jioni.

"Kiungo wa kimataifa wa Ujerumani Kai Havertz amejiunga nasi kutoka Chelsea kwa mkataba wa muda mrefu," Arsenal ilitangaza Jumanne.

Baada ya kujiunga na klabu hiyo ya Kaskazini mwa London, Havertz alizungumza kuhusu matumaini yake makubwa ya kupata mafanikio mengi pamoja na wachezaji wenzake wapya.

Alibainisha kuwa timu hiyo imepania kushinda mengi huku akidokeza kuwa hiyo ni sababu mojawapo iliyomfanya kukubali uhamisho huo.

"Lengo ni kushinda mataji na nitatoa kila kitu kufanya hivyo kwa wafuasi na kila mtu kwenye kilabu. Sasa ninatazamia kukutana na wachezaji na wengine wote tutakaporejea kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya,” alisema Havertz.

Mkurugenzi wa Michezo wa Arsenal, Edu alimsifu mchezaji huyo kijana akibainisha kuwa yeye ni nyongeza muhimu kwa klabu.

"Kama kijana mwenye uzoefu wa miaka 24, usajili wake unawakilisha hatua nyingine muhimu katika kuimarisha kiini chetu cha wachezaji wenye vipaji ambao tunao Arsenal. Tunatarajia kufanya kazi na Kai,” alisema Edu.

Kocha wa klabu hiyo Mikel Arteta alimkaribisha mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani na kusema kwamba yuko tayari kufanya kazi naye.

“Kai ni mchezaji wa ubora wa juu. Ana uwezo mkubwa wa kucheza na ni mchezaji mwenye akili. Ataleta kiasi kikubwa cha nguvu ya ziada kwenye safu yetu ya kiungo na aina mbalimbali za uchezaji wetu,” Arteta alisema.

Washindi hao wa pili wa EPL msimu wa 2022/23 wanaripotiwa kumsajili fowadi huyo mwenye umri wa miaka 24 kwa pauni milioni 65.

Kwa upande mwingine, siku ya Jumanne, West Ham pia walimpa nahodha wao Declan Rice idhini ya kufanyiwa vipimo vya afya na Arsenal baada ya kuafikiana nao kuhusu uhamisho.

West Ham inaripotiwa kukubali  ofa ya pauni milioni 105 kutoka kwa klabu hiyo ya Kaskazini mwa London na klabu zote mbili sasa zinashughulikia muundo wa malipo kabla ya Rice kusaini rasmi mkataba.