Kocha wa PSG Christophe Galtier akamatwa

Galtier alikamatwa pamoja na mtoto wake John Valovic-Galtier mwendo wa asubuhi kufuatia madai ya ubaguzi.

Muhtasari

•Kocha wa PSG, Christophe Galtier alizuiliwa kwa mahojiano siku ya Ijumaa kama sehemu ya uchunguzi wa madai ya ubaguzi.

•Madai ya ubaguzi dhidi ya Galtier yaliibuka kwa mara ya kwanza kwenye vyombo vya habari vya Ufaransa mwezi Aprili mwaka huu.

Kocha Christophe Galtier
Image: HISANI

Maafisa wa Polisi nchini Ufaransa walimzuilia kocha wa Paris Saint Germain (PSG), Christophe Galtier kwa mahojiano siku ya Ijumaa kama sehemu ya uchunguzi wa madai ya ubaguzi.

Mwendesha mashtaka wa Nice mnamo Ijumaa alithibitishia AFP kwamba Galtier alikamatwa pamoja na mtoto wake John Valovic-Galtier mwendo wa asubuhi. Kulingana na stesheni ya runinga ya Ufaransa ya RMC Sport, wawili hao waliwekwa chini ya ulinzi wa polisi mwendo wa saa tatu kasorobo asubuhi ya Ijumaa.

Hatua hiyo inafuatia uchunguzi ulioanzishwa mwezi Aprili, kufuatia madai kwamba kocha huyo alitoa matamshi ya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu kuhusu wachezaji alipokuwa akihudumu kama mkufunzi wa klabu ya Nice katika msimu wa 2021/22.

Mwendesha mashtaka alisema watatoa taarifa zaidi kuhusu kukamatwa kwa Galtier na mwanawe John kupitia taarifa baadaye siku ya Ijumaa.

Wakati akiwa na PSG baada ya kuchukua mikoba Julai 2022, wababe hao wa Ufaransa walichapwa mara 10 mwaka wa 2023 na kubandukiwa kwenye Ligi ya Mabingwa katika hatua ya 16 bora.

Madai ya ubaguzi dhidi ya Galtier yaliibuka kwa mara ya kwanza kwenye vyombo vya habari vya Ufaransa mwezi Aprili mwaka huu.