Cesar Azpilicueta: Nahodha wa Chelsea aondoka baada ya kuichezea miaka 11

Azpilicueta amemaliza miaka 11 akiwa na klabu hiyo na anatarajiwa kujiunga na Atletico Madrid.

Muhtasari

•Beki huyo wa Uhispania mwenye umri wa miaka 33 alijipatia sifa kila iliohitajika katika uwanja wa Stamford Bridge.

•Azpilicueta alikuwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake Chelsea.

Image: BBC

Nahodha wa Chelsea Cesar Azpilicueta amemaliza miaka 11 akiwa na klabu hiyo na anatarajiwa kujiunga na Atletico Madrid.

Beki huyo wa Uhispania mwenye umri wa miaka 33 alijipatia sifa kila iliohitajika katika uwanja wa Stamford Bridge, ikiwa ni pamoja na mataji mawili ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa.

Azpilicueta alikuwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake Chelsea.

"Ni vigumu kueleza jinsi ninavyohisi, ni ajabu," alisema.

Katika video ya mtandao wa kijamii iliyotumwa na klabu hiyo, Azpilicueta aliyekuwa akibubujikwa na machozi aliongeza: "Ninahisi nilitoa kila kitu. Naipenda.

"Nadhani itakuwa wazi sana kuchagua wakati bora zaidi wa maisha yangu, tuliposhinda Ligi ya Mabingwa huko Porto. Lilikuwa kombe langu la kwanza kama nahodha.

"Chelsea ni nyumbani kwangu, itakuwa hivyo kila wakati na natumai ninaweza kurejea katika nafasi tofauti."

Azpilicueta alianza na klabu ya utotoni ya Osasuna na akakaa miaka miwili Marseille kabla ya kukamilisha uhamisho wa £6.5m kwenda Chelsea mnamo Agosti 2012.