SOKA KIMATAIFA

Austin Jay Jay Okocha ateuliwa waziri wa michezo Nigeria

Alishiriki kwenye ligi tofauti kutoka 1993 hadi 2008 alipostaafu kwenye soka

Muhtasari

• Okocha amewahi kucheza katika ligi kuu za Ujerumani, Uturuki, Ufaransa, Uingereza miongoni mwa ligi zingine.

• Okocha ambaye anakumbukwa kwa weledi wake wa chenga za dharau  alistaafu soka mwaka wa 2008.

Image: HISANI

Aliyekuwa nyota wa soka duniani raia wa Nigeria Austin Azuka Okocha maarufu Jay- Jay Okocha ameteuliwa kuwa waziri mpya wa michezo nchini Nigeria.

Shujaa huyo mwenye umri wa miaka 50 alikuwa akicheza kama kiungo mshambulizi alisaidia timu yake ya Nigeria kunyakuwa mataji kadhaa alichezea timu ya taifa mara 73 kati ya mwaka 1993 na 2006.

Okocha alifungia Nigeria magoli 14 na alitajwa kushiriki katika kombe la ulimwengu mara tatu, huku akitambuliwa kama mmoja wa mashujaa wa soka bara la Afrika.

Gwiji huyo wa kabumbu alishiriki katika ligi tofauti tangu alipoanza na Enugu Rangers nchini Nigeria kabla ya kuelekea Borussia Neunkirchen Ujerumani Julai 1990.

Katika mwaka wa 1998, Paris Saint-Germain walitumia kima cha pauni milioni 14 kuzinasa huduma za gwiji huyo, ambapo klabu hiyo ilimfanya kuwa mchezaji ghali zaidi wa Afrika wakati huo.

Alitia saini ya kandarasi ya miaka minne na PSG, ambapo alishiriki katika mechi 84 na kutia wavuni mabao 12. Okocha pia ametambuliwa kuwa mwelekezi mwema wa mwanasoka Ronaldinho wa Brazil, wakati walikutana PSG.

Baadhi ya ligi zingine ambazo Okocha amewahi kushiriki ni pamoja na; Bundesliga ya Ujerumani, Turkish Super League ya Uturuki, French League 1 ya Ufaransa, English Premier League ya Uingereza, EFL Championship ya Uingereza pamoja na Qatar Stars League ya bara Asia kabla ya kustaafu kwake kutoka soka mwaka wa 2008.

Inasadifu kuwa mwanasoka huyo alishiriki kwenye soka na hatimaye licha ya kustaafu kwake taifa hilo limemkumbuka na kumpa wizara ya michezo huku viongozi katika taifa hilo wakitamani kufanya vyema zaidi katika sekta ya michezo.