Mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia watalazimika kucheza mechi zao zote za Caf Champions League nje ya nchi.
K’Ogalo ilijipata katika hali ya kutatanisha baada ya shirikisho la soka barani Afrika, Caf, kuondoa viwanja vyote nchini kwenye orodha ya viwanja vinavyoruhusiwa kucheza michuano za shirikisho hilo.
Tanzania ndiyo nchi pekee ya Afrika Mashariki iliyo na viwanja vilivyoidhinishwa, kulingana na orodha iliyotolewa na shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Cairo Jumapili.
Gor ilijihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya bara baada ya kunyakua taji la Ligi Kuu ya Kenya katika siku ya mwisho ya kampeni iliyokuwa na upinzani mkali kutoka kwa mahibu wao wa jadi Tusker.
Katibu Mkuu wa K’Ogalo, Sam Ocholla, alifichua Jumapili kwamba Shirikisho la Soka Tanzania lilikubali kuwaruhusu mababe hao wa jadi wa Kenya kucheza michezo yao ya awali na ya hatua ya makundi kwenye viwanja vya Azam na Benjamin Mkapa.
Ijapokuwa Gor wamewasiliana na Shirikisho la Soka la Kenya, Ocholla ana shaka kwamba bodi inayosimamia eneo hilo itaweza kutatua suala hilo kwa haraka.
Kenya ilipata shida kubwa mnamo 2021 wakati Uwanja wa Moi, Kasarani, na Nyayo Stadium ulizuiwa kuandaa michezo ya kimataifa.
Wakati wa kutathmini vifaa viwili vya Kenya kwa mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia la Fifa 2022, Kamati ya Ukaguzi ya Caf ilitamka kuwa hayaridhishi.
Kwa kukosekana kwa vifaa vya kutosha, vilabu vya Kenya vitalazimika kuandaa mechi za nyumbani katika nchi jirani. Matukio ya hivi punde yanamaanisha kuwa wawakilishi wa nchi katika Kombe la Mashirikisho la Caf, Kakamega Homeboyz, pia watawakaribisha wapinzani wao katika viwanja vya nje ya nchi.