Wizara ya michezo nchini inakaribisha zabuni kwa mapendekezo ya kukarabati na kuboresha viwanja vitatu nchini ili kufikia viwango vya shirikisho la soka barani, CAF.
Sports Kenya katika notisi kwenye tovuti yao, iliwataka wanakandarasi nchini kuwasilisha maombi ya kukarabati viwanja vitatu nchini ambavyo serikali inapania kutumia kama itapata kuwa mwenyeji wa AFCON 2027.
Mwezi Aprili Kenya iliwasilisha ombi la pamoja na taifa za Afrika Mashariki, Uganda na Tanzania ya kutaka kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027 . Viwanja hivi ambavyo wizara inataka ikarabatiwe ndivyo ambayo serikali inapania kutumia ikiwa ombi lao litakubaliwa.
Awali waziri wa michezo, Ababu Namwamba alikuwa amebainisha kuwa serikali ilikuwa tayari kutumia zaidi ya shilingi bilioni 4 kukarabati viwanja nchini kama mpango wa kuboresha viwango vya soka.
Viwanja hivyo vitatu ni uwanja wa kimataifa wa Moi Kasarani, Uwanja wa kitaifa wa Nyayo na uwanja wa Kipchoge Keino mjini Eldoret.
Tangazo hili la Sports Kenya unakuja siku moja baada ya Gor Mahia kutangaza watakuwa wenyeji wa mechi zao za CAF champions League nchini Tanzania kutokana a ukosefu wa viwanja vilivyoidhinishwa na shirika hilo nchini Kenya.
K’Ogalo ilijipata katika hali ya kutatanisha baada ya shirikisho la soka barani Afrika, Caf, kuondoa viwanja vyote nchini kwenye orodha ya viwanja vinavyoruhusiwa kucheza michuano za shirikisho hilo.
Tanzania ndiyo nchi pekee ya Afrika Mashariki iliyo na viwanja vilivyoidhinishwa, kulingana na orodha iliyotolewa na shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Cairo Jumapili.
Katibu Mkuu wa K’Ogalo, Sam Ocholla, alifichua Jumapili kwamba Shirikisho la Soka Tanzania lilikubali kuwaruhusu mababe hao wa jadi wa Kenya kucheza michezo yao ya awali na ya hatua ya makundi kwenye viwanja vya Azam na Benjamin Mkapa.