Aliyekuwa kipa wa Man United, Edwin van de Sar azungumzia afya yake baada ya kutolewa ICU

van der Sar alilazwa katika hospitali moja nchini Uholanzi siku kadhaa zilizopita kufuatia kuvuja damu kwenye ubongo.

Muhtasari

•Edwin van der Sar amevunja ukimya baada ya kutolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) alikokuwa amelazwa kwa siku kadhaa.

•Alichukua fursa hiyo kuwashukuru watu waliosimama naye alipokuwa amelazwa katika ICU na wale waliomtakia afueni ya haraka.

Image: TWITTER// EDWIN VAN DER SAR

Kipa wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Uholanzi Edwin van der Sar amevunja ukimya baada ya kutolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) alikokuwa amelazwa kwa siku kadhaa.

Mwanasoka huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 52 alilazwa katika hospitali moja nchini Uholanzi siku kadhaa zilizopita kufuatia kuvuja damu kwenye ubongo. Awali alilazwa katika hospitali ya Split akiwa likizoni nchini Croatia.

Katika taarifa ya siku ya Jumanne, van der Sar alisema atasalia hospitalini kwa siku kadhaa huku akiendelea kupata nafuu na kwamba anatumai kuruhusiwa kwenda nyumbani wiki ijayo.

"Nina furaha kushiriki kwamba siko tena katika chumba cha wagonjwa mahututi. Walakini, bado niko hospitalini. Natumai kurejea nyumbani wiki ijayo na kuchukua hatua inayofuata katika kupona kwangu!,” van der Sar alisema siku ya Jumanne jioni.

Aliambatanisha taarifa hiyo na picha yake na mkewe wakiwa kwenye kitanda cha hospitali. Katika picha, wote wawili walivaa tabasamu kubwa kwenye nyuso zao.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa zamani wa Ajax alichukua fursa hiyo kuwashukuru watu waliosimama naye alipokuwa amelazwa katika ICU na wale waliomtakia afueni ya haraka.

“Tunataka kumshukuru kila mtu kwa jumbe zote nzuri na za sapoti,” alisema kipa huyo wa zamani wa Manchester United na Ajax.

Taarifa hiyo ilikuwa mawasiliano ya kwanza ya moja kwa moja ya van der Sar tangu apatikane na damu kwenye ubongo akiwa nchini Croatia mnamo Julai 7 na kulazwa katika ICU huko. Hapo awali, mkewe na Ajax walikuwa wametoa taarifa kuhusu hali yake.