“Nitakuwa PSG hata bila ya mapenzi yenu” Neymar kwa mashabiki waliomtaka kuondoka

Mwishoni mwa msimu uliokamilika kundi la mashabiki watoro wa PSG waliingia nyumbani kwake kwa fuji nchini Ufaransa wakimtukana vibaya na kumtaka kuondoka katika klabu yao.

Muhtasari

• Neymar mpaka sasa ndiye anayeshikilia rekodi ya uhamisho wa hela ndefu Zaidi katika soka la kisasa.

• PSG walizama mfukoni mwaka 2017 ambapo walitoa kima cha Euro 222 kwa Barcelona, rekodi ambayo haijapata kuvunjwa hadi sasa.

Neymar Junior
Neymar Junior
Image: BBC

Mchezaji wa kimataifa wa Brazili na klabu ya PSG ya Ufaransa Neymar Jr ameweka wazi kuhusu mustakabali wake katika klabu hiyo.

Neymar ambaye alikosa sehemu kubwa ya msimu uliokamilika kutokana na msururu wa majeraha amesema kwamba yeye anaona mustakabali wake ukiwa bado katika klabu hiyo licha ya kwamba mashabiki hawamtaki.

Akizungumza na Caze TV, Neymar alisema kwamba anatumai msimu kesho atashiriki katika kampeni ya PSG kwa kile alisema kwamba bado ana mkataba nao na hajaambiwa chochote kuhusu kutemwa kwake au kuuzwa kwenda kwa timu nyingine.

Neymar pia aliwapa ujumbe mashabiki walioingia nyumbani kwake mwishoni mwa msimu kwa fujo wakimpa ujumbe wa kuondoka katika timu yao, akisema kuwa hata bila ya mapenzi yao kwake, bado tu ataisakatia PSG.

“Natumai mustakabali wangu bado utakuwa PSG msimu kesho. Niko na mkataba na hakuna mtu yeyote ameniambia kitu chochote kuhusu kuondoka. Hata kama hakuna mapenzi makubwa baina yangu na mashabiki, bado nitakuwepo PSG, na mapenzi yao au bila mapenzi yao,” Neymar alisema.

Mchezaji huyo amekuwa akihusishwa na uhamisho kwenda vilabu vingi tu vya ligi kuu ya Uingereza ikiwemo Chelsea na Manchester United.

Neymar mpaka sasa ndiye anayeshikilia rekodi ya uhamisho wa hela ndefu Zaidi katika soka la kisasa.

PSG walizama mfukoni mwaka 2017 ambapo walitoa kima cha Euro 222 kwa Barcelona, rekodi ambayo haijapata kuvunjwa hadi sasa.

Msimu ambao umekamilika ulikuwa mbaya kwake haswa katika kipindi cha pili, pindi baada ya kuondoka katika mashindano ya kombe la dunia ambapo Brazili walitemwa kwa matuta ya penalty ya Croatia katika awamu ya robo fainali.