Shabiki wa Burnley akamatwa kwa kumtupia kiberiti usoni beki wa Man City mechi ikiendelea

Lewis alibaki ameshika kichwa baada ya kitu kilichorushwa kutoka kwa mashabiki kutua usoni mwake.

Muhtasari

•Tukio hilo lilitokea baada ya Lewis kuanguka chini alipokuwa akipigania mpira na beki wa Burnley Conor Roberts kwenye ukingo mmoja wa uwanja wa Tuff Moor.

•Burnley ilipoteza mechi yake ya kwanza baada ya kurejea Ligi Kuu kwa washindi wa EPL 2022/23 kwenye uwanja wao wa nyumbani 

alitupiwa kiberiti katika kipindi cha kwanza cha mechi ya Burnley vs Man City Ijumaa jioni.
Rico Lewis alitupiwa kiberiti katika kipindi cha kwanza cha mechi ya Burnley vs Man City Ijumaa jioni.
Image: SKY SPORTS

Shabiki wa Burnley FC alitambuliwa na kutolewa nje ya uwanja siku ya  Ijumaa jioni baada ya mlinzi wa Manchester City Rico Lewis kugongwa na kiberiti cha chuma usoni wakati wa kipindi cha kwanza cha mechi ya ufunguzi wa EPL msimu wa 2023/24.

Tukio hilo lilitokea baada ya Lewis kuanguka chini alipokuwa akipigania mpira na beki wa Burnley Conor Roberts kwenye ukingo mmoja wa uwanja wa Tuff Moor. Wakati Roberts akijitetea kutokuwa na hatia, Lewis aligongwa na kiberiti cha chuma usoni alipokuwa akijaribu kuamka tena.

Beki huyo Mwingereza mwenye umri wa miaka 18 alibaki ameshika kichwa baada ya kitu kilichorushwa kutoka kwa mashabiki kutua usoni mwake.

Wakati mechi ya ufunguzi wa msimu ikiendelea, Burnley alilaani kitendo hicho na kuthibitisha kuwa aliyehusika ametambuliwa na kuondolewa uwanjani na polisi.

Katika taarifa yake, klabu hiyo ambayo ilikuwa ikicheza mechi yake ya kwanza baada ya kupandishwa daraja na kurudi katika Ligi Kuu ya Uingereza ilidokeza kwamba shabiki huyo atapigwa marufuku kuhudhuria mechi.

"Tunafahamu tukio lililotokea katika kipindi cha kwanza cha mechi ambapo kifaa kiilirushwa kwa mchezaji wa Manchester City Rico Lewis," taarifa ya Burnley ilisoma.

“Hili halikubaliki. Aliyehusika ametambuliwa na kuondolewa uwanjani na polisi. Mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kurusha chochote ndani ya uwanja atapokea agizo la kupigwa marufuku,” klabu hiyo ilisema.

Burnley ilipoteza mechi yake ya kwanza baada ya kurejea Ligi Kuu kwa washindi wa EPL 2022/23 kwenye uwanja wao wa nyumbani katika mechi iliyohudhuriwa na zaidi ya mashabiki 20,000. Clarrets walipambana sana lakini hawakuweza kufunga hata bao moja dhidi ya vijana wa Pep Guardiola ambao waliondoka na ushindi wa 0-3.

Mfungaji bora wa msimu uliopita, Erling Haaland alifanikiwa kufunga mabao mawili kwenye mechi hiyo ya ufunguzi wa msimu huku kiungo Rodrigo akifunga bao la tatu la Man City.

Fowadi wa Burnley Anass Zaroury pia alionyeshwa kadi nyekundu katika kipindi cha pili baada ya kucheza vibaya dhidi ya mlinzi wa City Kyle Walker.