Meneja wa timu ya Manchester City Mhispania Pep Guardiola katika mahojiano na wanahabari amefichua kwamba timu hiyo ilikuwa inamezea mate sana huduma za beki wa Uingereza Harry Maguire.
Guardiola alisema kwamba enzi hizo Maguire akiwa ndio wa kutegemewa katika mnara wa nyuma wa Leicester City, Manchester City walikuwa wanazitamani sana huduma zake lakini hawakuweza kufika bei na hivyo mahasimu wao wa tangu jadi Manchester United wakaziwahi huduma zake.
Kando na Manguire, Guardiola pia amefichua kwamba timu yake ilikuwa inazitaka huduma za beki wa Chelsea Marc Cucurella ambaye alikuwa Brighton kipindi hicho bila kumsaza Alexis Sanchez kipindi hicho akiwa Arsenal na aliyeishia kwenda Man United.
“Tulimtaka Harry Maguire na hatukumsajili kwa sababu hatukutaka kulipa ada inayotakiwa. Tulimtaka Cucurella, hatukulipa. Tulimtaka Alexis Sanchez, hatukulipa. Mwishowe, tutalipa kile kilicho sawa".
Maguire baada ya kuingiwa Manchester United, alishuka pakubwa katika viwango vyake vya mchezo kiasi kwamba kila tukio baya lililokuwa linatokea katika United lilikuwa linasukumwa kwake, si kutoka kwa wachezaji wenzake, mashabiki hadi waandishi wa habari.
Kabla ya kung’oa nanga kwa msimu huu, meneja Erik Ten Hag alimvua Maguire unahodha na kumpa Mreno Bruno Fernandes.
Maguire alikuwa anahusishwa kuondoka United ikisemekana kwamba meneja Ten Hag hana mpango naye tena katika kikosi chake lakini mchezaji huyo amesisitiza kwamba yuko tayari usalia United ili kuipambania nafasi yake katika kikosi cha Mholanzi huyo.
Hivi majuzi, timu ya West Ham ilionesha nia kuu ya kumsajili kutoka United kwa dau la pauni milioni 30.
Dau hilo lilikubaliwa na United ambao kwa dalili zote hawamtaki Maguire kuendelea nao lakini upande wa mchezaji ulidinda na kukataa wakisema kwamba West ham ni timu ndogo kwa Maguire amabye alihitaji kujiunga na timu kubwa.
Wakati ananunuliwa kutoka Leicester City kwenda United, Maguire aliweka rekdoi ya kuwa kipa ghali Zaidi Uingereza, akinunuliwa kwa dau la Zaidi ya pauni milioni 80.